Connect with us

Soka

Yanga sc Bado Kidogo

Matumaini ya klabu ya Yanga sc kufuzu hatua ya robo fainali ya michuano ya klabu bingwa barani Afrika bado yanatia shaka mpaka pale itakapopata ushindi wake wa kwanza katika michuano hiyo baada ya jana kulazimishwa sare ya 1-1 ugenini na Medeama Fc ya nchini Ghana.

Yanga sc sasa imefikisha alama mbili katika michezo mitatu baada ya kupata sare mbili mfululizo za matokeo ya 1-1 ikiwemo ya wiki iliyopita nyumbani dhidi ya Al Ahly Fc katika dimba la Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.

Kama ilivyokua katika mechi dhidi ya Al Ahly ambapo Yanga sc ililazimika kusawazisha bao la uongozi la Percy Tau ndivyo pia ilivyokua katika mchezo huo wa tatu uliofanyika jijini Kumasi nchini Ghana ambapo Pacome Zouzou alisawazisha bao la dakika ya 27 la Jonathan Sowah.

Medeama fc ilianza mchezo kwa kasi kubwa hali iliyowafanya Yanga sc kushindwa kufanya mashambulizi yake kama ilivyozoeleka lakini baadae kuanzia dakika ya 10 ya mchezo waliendelea na umiliki wa mpira kama kawaida yao huku uwepo wa mabeki watatu wa kati ukiwapa uhai wa kutosha.

Clement Mzize na Kennedy Musonda bado wanaonekana hawana maelewano ya kutosha eneo la mbele la ushambuliaji kiasi cha kushindwa kutunza mpira hasa wakati wa kujenga mashambulizi langoni mwa wapinzani.

Yanga sc walipata bao kupitia kwa Nickson Kibabage japo mwamuzi alikataa bao hilo huku akiwabeba wenyeji baada ya Kibabage kuchezewa faulo ya kadi nyekundi lakini mwamuzi alitoa kadi ya njano.

Sasa Yanga sc inarejea katika uwanja wa Benjamini Mkapa Disemba 20 kuwavaa Medeama Fc katika mchezo wa raundi ya nne ambapo mpaka sasa msimamo wa kundi D unaonyesha yeyote ana nafasi ya kushinda hasa baada ya sare ya Al Ahly na Cr Belouzdad.

Click to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

More in Soka