Mshambuliaji wa klabu ya Pyramid Fc Fiston Mayele ameivusha klabu hiyo kwenda hatua ya fainali ya michuano ya kombe la Klabu bingwa barani Afrika baada ya kufunga mabao mawili katika ushindi wa 3-2 dhidi ya Klabu ya Orlando Pirates ya Afrika Kusini.
Mchezo huo uliofanyika katika uwanja wa kimataifa wa Cairo ulishuhudiwa Pyramid Fc ikiruhusu bao la mapema kipindi cha kwanza dakika ya 41 likifungwa na winga raia wa Afrika kusini Relebohile Mofokeng lakini Mayele alisawazisha katika dakika za nyongeza za kipindi cha kwanza.
Kipindi cha pili dakika ya 52 Orlando Pirates walifanya shambulizi zuri na kufunga bao la pili kupitia kwa Nkong lakini bao hilo lilidumu kwa dakika tano pekee ambao Mohammed Sobhi alisawazisha dakika ya 57 na kuufanya mchezo kuwa sawa.
Wakati Pirates wakiamini kuwa wanaweza kufuzu fainali hizo ndipo Mayele alipounganisha mpira mgumu wa krosi ambao ulizama wavuni moja kwa moja dakika ya 85 ya mchezo huo ambapo baada ya mwamuzi kujiridhisha kupitia Teknolojia ya VAR aliamuru mpira uwekwe kati.
Mpaka dakika 90 zinamalizika Mayele aliibuka shujaa akiiongoza timu yake kufuzu fainali ambapo itakutana na Mamelod Sundowns iliyoitoa klabu ya Al Ahly Fc.