Bondia Muingereza Tyson Fury ambaye ni bingwa wa dunia wa WBC uzito wa juu amempiga kwa mara ya pili mfululizo bondia kutoka Marekani Deontay Wilder katika pambano lao la tatu kimkataba lilofanyika asubuhi hii Las Vegas Marekani na kuendeleza rekodi yake ya kutopoteza mchezo wowote.
Fury alimmaliza Wilder katika raundi ya 11 kwa KO na kutetea mkanda wake wa WBC katika moja ya pambano bora kabisa la masumbwi kuwahi kushuhudiwa hivi karibuni huku mastaa mbalimbali wakimwagia sifa kemkem bondia huyo.
Deontay Wilder amekimbizwa hospitali baada ya pambano hilo kwa uchunguzi zaidi wa afya baada ya kupokea makonde mazito kutoka kwa Fury,hata hivyo Fury amemsifu mpinzani wake kuwa na ngumi nzito zilizomchanganya mara kwa mara wakati pambano linaendelea.
Kwasasa ni rasmi ubishani wa mabondia hao umemalizika baada ya kutamatika kwa mapambano matatu yaliyokuwa katika mkataba wao ‘trilogy’ huku Tyson Fury akishinda mawili na moja kwenda sare.
Licha ya kupoteza kwa Aleksandr Usyk wapenzi wa ngumi duniani bado wana hamu ya kushuhudia pambano katika ya Anthony Joshua na Tyson Fury siku za usoni.