Kampuni ya PAF Promotion imemfungulia shauri la madai Bondia Hassan Mwakinyo ambalo linatarajiwa kutajwa kwa mara ya kwanza Novemba 13, 2023 katika Mahakama ya Hakimu mkazi Kisutu jijini Dar es salaam.
Katika shauri hilo lililosambaa mitandaoni linaonyesha kuwa baadhi ya madai yanamtaka Mwakinyo aombe radhi kwa kugoma kupanda ulingoni Septemba 29, 2023 na kutoa taarifa za uongo kupitia vyombo vya Habari ambazo taarifa hizo zimeichafua kampuni hiyo.
Mengine ni kulipa fidia Tsh. Milioni 142.5 (hasara ya kukosa mapato), kurejesha Tsh. Milioni 7.4 alizopokea, kulipa Tsh. Milioni 8 (gharama ya ukumbi), Tsh. Milioni 1.2 (malazi ya bondia mpinzani), Tsh. Milioni 3.8 (gharama za tiketi za ndege za mpinzani na wasaidizi wake) na faini ya Tsh. Milioni 150 (madhara ya jumla).
Awali Mwakinyo aligoma kupanda ulingoni katika pambano dhidi ya Julius Indongo siku ya septemba 26 kwa madai ya kwamba promota wa pambano hilo kampuni ya Paf Promotions imekiuka baadhi ya makubaliano katika mkataba.
Mbali na shauri hilo tayari Shirikisho la ngumi za kulipwa nchini limemfungia bondia huyo kutopanda ulingoni kwa muda wa mwaka mmoja pamoja na kulipa faini ya kiasi cha shilingi milioni moja za kitanzania.