Klabu ya Yanga sc imerejesha makali yake ya ufungaji baada ya kuifunga Fountain Gate Fc kwa mabao 5-0 katika mchezo wa ligi kuu ya Nbc nchini uliofanyika katika uwanja wa Kmc Complex uliopo Mwenge jijini Dar es Salaam.
Kocha Sead Ramovic ni kama ameshapata kikosi cha kwanza baada ya kuwaanzisha mastaa wale wale katika mechi nne mfululizo ambapo golini alianza AbouTwalib Mshery akisaidiwa na mabeki Kibwana Shomari,Shadrack Boka,Dickson Job na Ibrahim Hamad huku eneo la kiungo wakianza Khalid Aucho na Mudathir Yahaya sambamba na Stephan Aziz Ki na Prince Dube akiongoza safu ya ushambuliaji pamoja na Pacome Zouzoua na Clement Mzize.
Iliwachukua Yanga sc dakika 15 kupata bao la kwanza kupitia kwa Pacome Zouzoua aliyemalizia krosi ya Boka na mpira kumshinda kipa John Noble wa Fountain Gate.
Dakika za mwishoni mwa kipindi cha pili Pacome Zouzoua alifunga bao la pili akipokea pasi ya Mzize ndani ya box la Fountain Gate huku pia Kona safi ya Aziz Ki ilisetiwa vizuri na Dube kisha mpira kumkuta Mudathir Yahaya aliyefunga bao la tatu kwa Yanga sc mabao ambayo yalidumu mpaka mapumziko.
Kipindi cha pili Yanga sc iliendeleza moto wa Gusa achia twende kwao ambapo Pacome Zouzoua aliwatoka walinzi wa Fountain Gate na kupiga shuti kali liligonga mwamba na kumgonga beki Ramadhan Shiga dakika ya 52 ya mchezo.
Baada ya kupata idadi hiyo ya Magoli kocha Ramovic aliwapumzisha Khalid Aucho na Prince Dube huku akiwaingiza Farid Mussa na Duke Abuya.
Clement Mzize aliwanyanyua mashabiki wa Yanga sc kwa furaha dakika ya 88 akimchungulia kipa John Noble na kufunga bao la tano kwa Yanga sc na bao la sita kwake msimu huu.
Kocha Ramovic ni kama ameshajipata klabuni hapo baada ya kufunga mabao 18 katika michezo mitano pekee la ligi kuu tofauti na mtangulizi wake Gamondi aliyefunga mabao 14 pekee katika michezo 10 ya ligi kuu ya Nbc.
Yanga sc sasa imefikisha alama 40 ikicheza michezo 15 ya ligi kuu ya Nbc nchini ikiwa katika nafasi ya pili ya msimamo wa ligi hiyo.