Klabu ya Yanga sc imefanikiwa kuchukua alama tatu katika mchezo wa ligi kuu ya Nbc nchini dhidi ya Klabu ya Tanzania Prisons uliofanyika katika uwanja wa Kmc Complex uliopo Mwenge jijini Dar es Salaam.
Katika mchezo huo ilishuhudiwa dakika tisini zikikamilika kwa Yanga sc kupata ushindi wa mabao 4-0 huku Ibrahim Bacca akiwa mchezaji bora wa mechi baada ya kufunga mabao mawili kati ya manne.
Clement Mzize alifungua kalamu ya mabao baada ya kupata pasi nzuri ya Prince Dube dakika ya 13 kisha Bacca aliunganisha mpira uliogonga mwamba wa Aziz Ki dakika ya 42 ya mchezo huo huku dakika tatu baadae Dube alifunga bao la tatu akipokea pasi ya Stephan Aziz Ki.
Baada ya Mapumziko Prisons iliamua kurudi nyuma na kuzuia ili isifungwe mabao mengi lakini walijisahau dakika ya 83 ya mchezo na kuruhusu bao la kichwa la Ibrahim Hamad Bacca na kufanya mchezo huo kumalizika kwa Yanga sc kupata mabao 4-0.
Kocha Sead Ramovic baada ya mchezo huo alisema kuwa ushindi huo umetokana na wachezaji wake kujituma dakika zote.
“Tulikuwa na mechi ngumu wote,nawapongeza wapinzani kwa mechi ngumu,tumeongeza fitness yetu na nyie wote mnaona sasa, najivunia kuwa kocha wa hii timu na kuongoza kundi hili la wachezaji na inshallah mwishoni tutakuwa na wakati nzuri.” Alisema Ramovic
Yanga sc sasa imefikisha alama 33 ikiwa nyuma ya Simba sc kwa alama moja baada ya kucheza michezo 13 ya ligi kuu ya Nbc nchini.