Connect with us

Soka

Dube Apiga “Hatrick” Vs Mashujaa Fc

Mshambuliaji wa klabu ya Yanga sc Prince Mpumelelo Dube amefungua rasmi akaunti ya mabao katika ligi kuu ya Nbc nchini baada ya kupachika mabao 3 katika ushindi wa 3-2 ilioupata klabu ya Yanga sc dhidi ya Mashujaa Fc.

Dube amefunga mabao hayo katika mchezo uliomalizika muda mchache uliopita katika uwanja wa Kmc Complex uliopo Mwenge jijini Dar es Salaam ambapo mshambuliaji huyo alicheza vizuri kuanzia dakika ya kwanza ya mchezo huku akitengeneza bao la kwanza kuanzisha shambulizi alilokuja kulimalizia kwa pasi nzuri ya Pacome Zouzoua dakika ya 7 ya mchezo.

Dakika ya 21 Dube alifunga bao la pili kwa kichwa akiunganisha mpira uliokolewa vibaya na mabeki wa Mashujaa Fc lakini Mashujaa Fc walirudi kwa nguvu na kufunga bao la kwanza dakika ya 45 kwa shuti kali kupitia kwa David Uromi na kumuacha kipa Abubakari Khomeini akiwa hana la kufanya.

Dube alifunga bao la tatu kwa kichwa akimalizia krosi ya Kibwana Shomari dakika ya 53 lakini dakika tisa baada makosa ya kipa Khomeini yaliwapa mashujaa Fc bao la pili kutokana na shuti la Idris Stambuli.

Mabadiliko ya kuwaingiza Mudathir Yahaya na Farid Musa sambamba na Shadrack Boka yaliwapa uimara Yanga sc ambao walikaza mpaka mwisho wa mchezo na kuzoa alama tatu muhimu.

Yanga sc sasa imefikisha alama 30 katika nafasi ya tatu ya msimamo wa ligi kuu ya Nbc nchini ikicheza michezo 12 mpaka sasa.

Click to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

More in Soka