Klabu ya Yanga sc inapaswa kutoa kiasi cha dola laki tano ili kumbakisha kiungo mshambuliaji Stephane Aziz Ki klabuni hapo la sivyo ataondoka mwishoni mwa msimu huu wa ligi kuu nchini utakapotamatika kutokana na ofa ambazo tayari anazo mkononi mwake mpaka sasa.
Aziz Ki ambaye alitua Yanga sc msimu wa 2022 ambapo alisaini mkataba wa miaka miwili ambao hivi sasa unaelekea tamati huku klabu yake ya Yanga sc ikiwa tayari imefanya majaribio kadhaa ya kumbakisha ambapo amekubali kubaki lakini dau la kumbakisha ni hilo ambalo kwa pesa za kitanzania linakadiriwa kufikia bilioni 1.2.
Mpaka sasa klabu za Mamelod Sundowns,Kaizer Chief,Al ahly na Zamalek Fc zote zimeonyesha nia ya kumsajili huku Kaizer Chiefs na Mamelod Sundowns zikiwa mstari wa mbele kuhakikisha kuwa zinamnasa kiungo huyo ambaye mpaka sasa amefunga mabao 16 ya ligi kuu akiwa na pia amesaidia upatikanaji wa mabao saba katika ligi kuu pekee.
Wakala wa mchezaji huyo Zambro Traore hivi karibuni aliwasili hapa nchini sambamba na mama mzazi wa Aziz Ki kwa ajili ya kujadili mkataba mpya ambapo mpaka sasa uamuzi upo kwa mabosi wa Yanga sc kuamua kulipa ama la.
Kwa hali ilivyo mpaka sasa ni ngumu kwa Yanga sc kulipa kiasi hicho cha pesa ikizingatiwa kuwa malipo hayo ni dau la usajili pekee huku mshahara na marupurupu mengine nayo yakidaiwa anahitaji yaongezeke ilhali hivi sasa anapokea mshahara unaokadiriwa kufikia kiasi cha dola elfu kumi kwa mwezi.