Bodi ya Ligi Kuu imeijibu barua iliyoandikwa na klabu ya Yanga sc ambayo ilikuwa inataka ipewe alama 3 na mabao 3 kwenye mchezo ulioahirishwa wa tarehe 8 Machi,2025 dhidi ya Simba Sc.
Yanga ilitaka ipewe alama hizo baada ya bodi ya ligi kuahirisha mchezo huo dhidi ya Simba Sc licha ya klabu hiyo kama mwenyeji kukamilisha taratibu zote za mchezo huo.
Katika barua ya tarehe 16 Machi,2025 yenye Kumb.Na TPLB/CEO/2024/625, Bodi imejibu barua hiyo ikisema kuwa mechi iliahirishwa kwa kufuata kanuni na wala sio kwa sababu Simba Sc waligomea mchezo kama ambavyo Yanga sc wanadai.
Katika barua hiyo ya Bodi yenye kurasa 3 na vipengele 12, Bodi imewaambia Yanga sc mchezo uliahirishwa rasmi saa 8 mchana baada ya hapo hakukuwa na taratibu zozote kuhusu mchezo huo ambazo ziliendelea huku maafisa wote wa mchezo ambao walikuwa wakifanya shughuli za mechi katika uwanja wa Benjamin Mkapa waliondoka isipokuwa wale wa usalama pekee.
“Hakukuwa na taratibu zozote za mchezo zilizoendelea kama zinavyoelezwa kwenye kanuni 17 ambazo zilifanywa ili kuipatia timu iliyopo kiwanjani alama 3 na mabao 3 kikanuni, ikiwemo kukagua timu hiyo”, inasomeka sehemu ya barua hiyo ya majibu kwa Yanga SC.
“Klabu yako inapaswa kuelewa kwamba kanuni za ligi Kuu namba 17:45 haisemi popote kwamba klabu mgeni (visiting team) inapaswa kuwasiliana na wadau wengine ili kutimiza takwa la kikanuni la wao kwenda kufanya mazoezi kwenye uwanja utakaochezwa mechi”, Imesomeka barua hiy ya bodi.
Pia bodi imesema waliita kikao cha dharura cha Kamati ya uendeshaji na usimamizi wa Ligi baada ya kupokea ripoti tofauti tofauti zenye mfululizo wa matukio uliojenga msingi wa mgogoro uliotokea tarehe 7 Machi,2025 pale Benjamin Mkapa wakati Simba sc wakitaka kufanya mazoezi.
Kutokana na umuhimu na unyeti wa taarifa zilizopokelewa, zingine zilitishia usalama, vitisho, tuhuma za rushwa, ambazo zinachukuliwa kwa umuhimu na upekee kwenye soka, Kamati iliona umuhimu wa kuhairisha mechi, ili kuepuka changamoto za kiusalama kabla hazijatokea, kabla au baada ya mechi, ili kujipa muda na pengine kuhusisha vyombo vya kitaifa vya uchunguzi,imesema barua hii ya Bodi kwenda Yanga sc
Kamati iliona matokeo hasi ya kuahirishwa mechi ni madogo kuliko matokeo hasi ambayo yangetokea kwa mechi hiyo kuchezwa.Aidha kwa kupeleka timu kiwanjani Yanga wamekiuka kanuni 47:18.
Mpaka sasa bado Yanga sc hawajajibu kama wataendelea na msimamo wa kutocheza mechi hiyo ama lah.