Klabu ya Yanga sc imefanikiwa kuibuka na ushindi wa alama tatu katika mchezo wa ligi kuu ya Nbc dhidi ya Dodoma Jiji uliofanyika katika uwanja wa Jamhuri jijini humo Mei 22 na kuzidi kujichimbia kileleni mwa msimamo wa ligi kuu nchini.
Iliwachukua Yanga sc dakika 10 pekee kuandika bao la kwanza kupitia kwa Clement Mzize baada ya kufanya majaribio kadhaa ya kupata bao ambapo krosi nzuri ya Joyce Lomalisa iliunganishwa kwa kichwa na Mzize na kuipatia Yanga sc bao la uongozi huku bao la pili likifungwa na Stephane Aziz Ki kwa penati baada ya yeye mwenyewe kuangushwa katika eneo la hatari na beki wa Dodoma Jiji dakika chache kabla ya mapumziko.
Dakika ya 51 Kibwana Shomari alitoa pasi nzuri kwa Mzize ambaye alimzidi maarifa beki wa Dodoma Jiji na mpira kumkuta Aziz Ki aliyefunga bao la tatu na la pili kwake katika mchezo huo huku Maxi Mpia Nzengeli ambaye aliingia kipindi cha pili alifunga bao la nne akipokea pasi nzuri ya Joseph Guede dakika ya 78 ya mchezo.
Yanga sc baada ya ushindi huo sasa imefikisha alama 74 juu ya msimamo wa ligi kuu huku tayari ikiwa imeshatangazwa kuwa mabigwa wa ligi kuu kwa mara ya 30 na watakabidhiwa kombe siku ya Mei 25 katika uwanja wa Benjamini Mkapa ambapo watakua na mchezo dhidi ya Tabora United.