Klabu ya Yanga sc imefanikiwa kuibuka na alama tatu katika mchezo wa ligi kuu ya Nbc nchini baada ya kuifunga Azam Fc kwa mabao 2-1 katika mchezo uliofanyika katika uwanja wa Chamazi Complex jijini Dar es salaam.
Yanga sc ikianza mchezo bila mastaa wake Stephan Aziz Ki aliyeanzia benchi Pamoja na Khalid Aucho ambaye ana majeraha ya nyama za paja ambapo Kocha Hamd Miloud aliamua kumuanzisha Pacome Zouzou Pamoja na Cletous Chama huku nafasi ya Aucho ikizbwa na Duke Abuya.

Prince Dube ambaye anawafahamu vizuri mabeki wa Azam Fc aliamua mchezo huo baada ya kuwasumbua vilivyo mabeki hao ambapo uimara wa kipa Zubeir Foba uliwaokoa Azam Fc mara kwa mara lakini dakika ya 11 alitoa pasi nzuri kwa Pacome Zouzoua na kufunga bao la kwanza kwa Yanga sc.

Foba aliendelea kuwaokoa Azam Fc akiokoa michomo kadhaa lakini Dube alifunga bao la pili dakika ya 34 akimchambua vizuri kipa huyo.
Mpaka mapumziki Yanga sc walikua wanaongoza kwa mabao 2-0 lakini kipindi cha pili waliamua kutulia na kupunguza kasi ya mchezo huo na kuwapa nafuu Azam Fc ambao walijitahidi kufanya mashambulizi kupitia kwa Feisal Salum na Idd Nado.

Yanga sc Pamoja na kuwaingiza Aziz Ki na Clement Mzize walipoza mashambulizi huku wakishambulia kwa kushtukiza wakiwaacha Azam Fc watawale mpira kwa muda mwingi ambapo dakika ya 81 ya mchezo Lusajo Mwaikenda alifunga bao la kufutia machozi kwa Azam Fc.
Dakika tisini za mwamuzi Ahmed Arajinga zilimalika kwa Yanga sc kuchukua alama tatu na kufikisha alama 67 kileleni mwa ligi kuu huku Azam Fc akisalia nafasi ya tatu na alama 51.