Wakati wapenzi wa soka nchini wakisubiria kwa hamu msimu mpya wa ligi kuu soka Tanzania Bara (TPL) inayotarajiwa kuanza mwishoni mwa mwezi wa tisa kutokana na usajili mkubwa uliofanya na vilabu mbalimbali vinavyoshiriki ligi hiyo,kuna jambo lingine la kuvutia zaidi ambayo ambapo tutashuhudia michezo mikoani kadhaa ikipigwa usiku.
Hilo linakuja kutokana na viwanja vinne vya mikoani vitakavyotumiwa na vilabu shiriki kuwa katika hatua mbalimbali za uwekaji wa taa za usiku viwanjani hapo.
Viwanja hivyo ni pamoja na Majaliwa stadium(Namungo fc), Jamhuri Dodoma(Dodoma Jiji na Tanzania Prisons),Kaitaba stadium(Kagera Sugar) na Mkwakwani Tanga(Coastal Union) ambavyo wakandarasi wanaendelea na kazi.
Ufungaji huo wa taa za viwanjani unapewa nguvu na wadhamini wa ligi hiyo Azam tv katika juhudi zao za kuhakikisha ligi hiyo inakuwa bora kuanzia mazingira ya viwanja wakati wa urushaji wa matangazo kwa njia ya televisheni.
Katika kufanikisha hilo Azam tv wanashirikiana na vilabu husika pamoja na wamiliki wa viwanja hivyo ambavyo vingi vipo chini ya Chama cha mapinduzi(CCM).Vilabu na wamiliki watapaswa kuweka nguvu zao katika kuweka misingi pamoja na majenereta ya kuwashia taa hizo huku Azam wakihusika zaidi na upandishaji wa minara na ufungaji wa taa zenyewe.
Azam watagharamia zaidi ya aslimia 70 za ujenzi wakati vilabu na wamiliki wakitakiwa kuchangia asilimia 25 tu za ujenzi.