Connect with us

Makala

Simba sc Yaipiga 3 SBS

Ni kama kusukuma mlevi tu ndivyo unavyoweza kusema baada ya klabu ya Simba sc kutumia nguvu kidogo tu kupata ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Singida Big Stars tofauti na ilivyotarajiwa na mashabiki wengi wa soka nchini katika mchezo uliofanyika katika uwanja wa Benjamini Mkapa jijini Dar es salaam.

Ikianza na straika mpya Jean Baleke akisaidiwa na Cletous Chama na Saido Ntibanzokiza Simba sc ilitawala eneo la kiungo na kuweka kambi langoni mwa Singida Big Stars huku Baleke akiandika bao la kwanza dakika ya nane ya mchezo akiunganisha krosi ya Chama.

Dakika ya 21 faulo iliyopigwa upande wa kulia ilimkuta Saido Ntibanzokiza ambaye aliunganisha mpira kwa kichwa na kufunga bao la pili kwa mnyama ambapo  Singida Big Stars walisawazisha dakika ya 35 kwa faulo ya Bruno Gomez na mpaka mapumziko matokeo yalikua 2-1.

Kipindi cha pili licha ya kosakosa za hapa na pale Pape Osmane Sakho alifunga bao la tatu kwa tiktak nzuri akimalizia krosi ya Shomari Kapombe na baada ya hapo Simba walitawala mchezo mpaka mpira unamalizika na kuwaacha Singida wakishangaa kutokana na kipigo hicho.

Kocha Hans Van Pluijm ni kama alitaka kufungwa kutokana na aina ya kikosi alichoanza nacho ambapo alianza na washambuliaji wawili Francy Kazadi na Meddie Kagere huku nyuma yao akiweka viungo wanne bila winga asilia hata mmoja na kuwapa kazi rahisi mabeki wa pembeni wa Simba sc Shomari Kapombe na Mohamed Hussein kupanda mara kwa mara.

Simba sc sasa imezidi kuipa presha Yanga sc baada ya kufikisha alama 53 nyuma ya Yanga sc yenye alama 56 ikiwa na mchezo mmoja mkononi huku Singida ikisaliwa na alama zake 43.

Click to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

More in Makala