Mastaa wapya wa Simba na Yanga Farouk shikalo na Francis Kahata wameng’aa katika usiku wa tuzo za ligi kuu nchini Kenya baada ya wawili hao kutwaa tuzo za kipa bora na kiungo bora kwa msimu wa ligi kuu ulioisha nchini humo.
Shikalo ametwaa tuzo hiyo baada ya kufanya vizuri alipokua Bandari Fc ya nchini humo huku Kahata ametwaa baada ya kuonyesha kiwango safi wakati akiitumika Gormahia ya nchini humo.
Licha ya kufanya vizuri katika ligi kuu pia wachezaji hao waliitwa katika kikosi cha Kenya kilichoshiriki michuano ya Afcon nchini Misri mwezi juni.
Wachezaji hao hivi sasa wanachezea Yanga na Simba za nchini baada ya kuhama timu zao za awali huku Shikalo akiwa na uhakika namba ya kudumu katika kikosi cha Mwinyi Zahera huku Kahata akihitaji kufanya kazi ya ziada ili kumshawishi kocha Aussems licha ya kufunga goli katika mchezo dhidi ya Azam na kuisaidia Simba sc kutwaa ngao ya jamii kwa mara ya tatu mfululizo.
Tuzo zingine za ligi hiyo zilibebwa na Josh Onyango aliyetwaa tuzo mbili ya beki bora na mchezaji bora wa ligi hiyo huku wafungaji bora wakiwa ni Enosh Ochieng(Ulinzi Stars),Allan Wanga (Kakamega Homeboys) na Umaru Kasumba (Sofapaka) huku David Majak wa Tusker Fc akitwaa tuzo ya mchezaji chipukizi na Kocha wa Gormahia Hassan Oktay akitwaa tuzo ya kocha bora.