Mvua iliyonyesha wakati wa mchezo wa Uzinduzi wa uwanja wa Airtel stadium mkoani Singida imesababisha kuvunjika kwa mchezo baina ya timu za Yanga sc dhidi ya Singida Black Stars.

Mchezo huo wa Uzinduzi ulivunjika dakika ya 67 ya mchezo huo kutokana na mvua kubwa iliyonyesha uwanjani hapo ambapo mwamuzi alilazimika kusimamisha mchezo huo kutokana na mvua hiyo pia kuambatana na upepo mkali.
Licha ya mvua hiyo kupungua baada ya takribani dakika 45 ilionekana ni vyema mchezo huo kuishia hapo ili kulinda afya za wachezaji.
Katika mchezo huo Yanga sc ilianza na kikosi tofauti kutokana na mastaa wake baadhi kuwa katika majukumu ya timu za Taifa ambapo Aboubakari Khomeini alianza golini akisaidiwa na Kibwana Shomari,Nickson Kibabage,Chadrack Boka na Aziz Andambwile na eneo la kiungo liliongozwa na Salum Abubakar,Jonathan Ikangalombo,Jonas Mkude na Pacome Zouzoua huku Maxi Nzengeli na Shekhan Ibrahim wakiongoza eneo la ushambuliaji.

Iliwachukua Yanga sc dakika 19 kupata bao la kwanza kupitia kwa Jonathan Ikangalombo lakini bao hilo lilisawazishwa dakika ya 56 na Serge Pokou.
Matokeo yalisalia hivyo hivyo kutokana na mwamuzi kumaliza mchezo huo kabla ya dakika 90 kumalizika.
Katika mchezo mgeni rasmi alikua ni Naibu Waziri wa sanaaa,utamaduni na michezo Mh.Hamis Mwinjuma.