Kocha Florent Ibenge amewasili na kikosi cha klabu yake ya Al Hilal kuja kuwavaa Yanga sc katika mchezo wa kimataifa wa kirafiki utakaofanyika katika uwanja wa Benjamin mkapa siku ya Jumamosi Octoba 10 jijini Dar es salaam.
Wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere kocha huyo raia wa Congo alisema wazi kuwa Yanga sc kwa sasa ni timu bora nchini zaidi ya Simba sc kutokana na aina ya wachezaji iliowasajili miaka ya hivi karibuni hasa wakina Fiston Kalala Mayele na wenzake ambao wengi anawafahamu uwezo wao.
“Tuko hapa kucheza vizuri kama inavyowezekana tukijua kama itakua mechi ngumu pia nawajua wachezaji wengi wa klabu ya Yanga sc kama Jesus Moloko,Morrison,Lomalisa Mutambala na wachezaji wengi waliocheza na mimi kama kocha wote ni wazuri na ndio maana nasema mchezo utakua mgumu maana Yanga sc ina wachezaji wazuri,Ni timu nzuri na ngumu lakini tuna imani kuwa tutashinda na kucheza vizuri”.
“Hali ya hewa ni nzuri joto sio kubwa kama Sudan japo linafanana na Lubumbashi na Tunajitahidi kujiboresha ndio maana tunacheza michezo ya kirafiki,Hii ni mara ya kwanza nacheza na Yanga sc na hii ni tofauti na Simba sc kwa sasa kwa maana wameongezeka ubora huku mpira wa Tanzania ukikua kutokana na kuja kwa wachezaji wazuri”.Alisema Ibenge ambaye aliwahi kuifundisha klabu ya As Vita akiwa na wachezaji kama Fiston Mayele na Djuma Shabani.
Pia kocha huyo aliulizwa kama anamhofia Mayele naye hakusita kusema kuwa “Kwa sasa ni muda wake japo sisi hatutamuangalia yeye pekee bali tutawaangalia kama timu kwa maana wapo wakina Hertier Makambo,Moloko na Morrison ambao wanaweza kuleta madhara”.
Mchezo huo unatarajiwa kuwa mkali na wa ushindani baina ya timu hizo huku mwamko wa mashabiki ukiwa juu hasa kutokana na klabu ya Yanga sc kuamua kuweka viingilio rafiki ambapo kiingilio cha juu kikiwa ni Shilingi Elfu 15 na kiingilio cha chini kikiwa ni shilingi elfu tatu tu.