Kocha wa klabu ya Al Hilal Omdurman Florent Ibenge amesema kuwa mchezo baina ya klabu yake dhidi ya Yanga sc ni mchezo mgumu lakini sio muhimu sans kwake kwa kuwa tayari ameshafuzu hatua inayofuatia ya robo fainali ya michuano ya klabu bingwa barani Afrika.
Mpaka sasa Al Hilal inaongoza kundi A la michuano hiyo ikiwa na alama 10 kileleni mwa msimamo ambapo kimahesabu tayari wamefuzu baada ya kupata ushindi katika michezo mitatu na sare moja huku wakikutana na Yanga sc siku ya Jumapili Januari 12 mwaka huu.
“Huu sio mchezo muhimu kwetu,ni mchezo muhimu zaidi kwa wapinzani wetu ndio maana utakuwa mchezo mgumu,sisi tunafurahi kuona tulitumia nguvu kubwa katika michezo ya mwanzo ambayo imepelekea kufuzu mapema”.
“Niwapongeze wachezaji wangu kwa kazi ngumu na kubwa waliyotumia katika michezo ya mwanzo naamini tulitumia nguvu na presha kubwa tofauti na michezo tunayoenda kucheza sasa haitakuwa na presha kubwa kwetu bali ni kwa wapinzani wetu”,Alimalizia kusema Ibenge kocha wa zamani wa vilabu vya As Vita na Rs Berkane.
Kwa upande wa Yanga sc ambao tayari wamewasili Mauritania kwa ajili ya mchezo huo wao wamesema kuwa hawana presha na mchezo huo.
”Tunaenda kwa Al Hilal kupata alama tatu, hatuna presha na hata msimu uliopita wachezaji walikutana na hali kama hii, sisi tunajiamini na tumejiandaa kurudi na alama tatu”.Alisema kocha msaidizi wa klabu hiyo Abdi Hamid Moalin.
Yanga sc inapaswa kushinda michezo yake miwili dhidi ya Al Hilal Omdurman na Mc Algers ili kufuzu robo fainali ya michuano hiyo mikubwa barani Afrika kwa ngazi za vilabu.