Ni mwanariadha wa kimataifa anayeshikilia rekodi ya dunia ya Olympic ya mbio za masafa marefu zaidi aliyoiweka huko Berlin Ujerumani mwaka 2018. Pia leo ametangazwa kuwa binadamu wa kwanza kukimbia mbio za Marathon na kuhitimisha chini ya masaa mawili huko Viena, Austria.
Amezaliwa mwaka 1984 kijiji cha Kapsisiywa, Kaunti ya Nandi, Rift Valley magharibi mwa Kenya. Ni mtoto wa mwisho kati ya watoto wanne wa Mwalimu Janeth Rotich. Amelelewa na mama yake tu (hamjui baba yake).
_
Alianza riadha tangu akiwa shule ya msingi. Na alipofika sekondari (Kaptel Secondary School) alikua akishiriki mashindano ya mita 2000. Alikutana na mkufunzi wake Patrick Sang (bingwa wa zamani wa Olympic) mwaka 2000 akiwa na miaka 16, ambapo amekua akimfua hadi sasa.
Mara ya kwanza kuweka rekodi ya dunia ni mwaka 2013 aliposhinda mbio za Hamburg Marathon kwa kutumia masaa mawili, dakika 5 na sekunde 30, kabla ya kuivunja rekodi hiyo mwaka uliofuata kwenye Chicago Marathon, kwa kutumia masaa mawili, dakika 4 na sekunde 11.
Tangu wakati huo Kipchoge amekuwa akiweka rekodi za dunia na kuzivunja mwenyewe. Ana mataji 13 ya marathon, na rekodi 6 za dunia, ambazo hazijawahi kuvunjwa na mtu mwingine. Baadhi ya rekodi hizo amezivunja mwenyewe.
Mapema mwaka huu Kipchoge aliweka azma ya kukimbia mbio za marathon chini ya masaa mawili. Lakini wataalamu kutoka Chuo kikuu cha Monash huko Melbourne, Australia walisema azma yake hiyo haiwezi kufanikiwa kwa sasa.
Taarifa iliyotolewa mwezi March mwaka huu, ilieleza kuwa utafiti uliofanywa na chuo hicho, unaonesha binadamu wa kwanza kukimbia Marathon kwa muda chini ya masaa mawili anaweza kupatikana mwaka 2032.
Licha ya taarifa hiyo Kipchoge aliendelea kujifua hadi leo alipoweka rekodi mpya huko Viena.
Kipchoge amemuoa Grace Sugutt na wana watoto watatu. Anatajwa kuwa na ukwasi wa $7M, karibu TZS Bil 15 za kitanzania, na kuwa mwanamichezo wa pili kwa utajiri Afrika Mashariki, akitanguliwa na Victor Wanyama mwenye $9M sawa na TZS Bil 20, akifutiwa na Mbwana Samatta mwenye $3M, sawa na TZS Bil 7.
Licha ya ukwasi huo, Kipchoge si mtu wa kupenda ufahari na anaishi maisha ya kawaida mjini Nairobi.!