Ikiwa bado na michezo mitatu mkononi klabu ya Yanga sc imefanikiwa kuibuka mabingwa wa ligi kuu ya soka ya Nbc nchini Tanzania baada ya kuifunga mabao 3-1 timu ya Mtibwa Sugar na kufanikiwa kufikisha alama 71 ambazo haziwezi kufikiwa na timu yeyote hapa nchini.
Yanga sc imefikisha alama hizo 71 katika michezo 27 ya ligi kuu nchini ambapo kwa wastani imefanikiwa kuzifunga walau mara moja timu zote 15 za ligi kuu nchini huku ikivuna mtaji mkubwa wa wastani wa mabao 47 ya kufunga na kufungwa.
Hesabu za Yanga sc kutwaa ubingwa ziliingia doa dakika ya 32 baada ya krosi ya Jimson Mwanuke kumkuta Charles Ilanfya ambaye alifunga kwa kichwa na kuandikia Mtibwa Sugar bao la uongozi ambalo lilidumu mpaka mapumziko.
Kennedy Musonda aliisawazishia Yanga sc bao akipokea pasi safi ya Mudathir Yahaya na kufunga bao zuri kwa mguu wa kushoto huku beki wa Mtibwa Sugar Nasri Kombo akijifunga bao la pili akiwa katika harakati za kuok0a.
Bakari Nondo Mwamnyeto alimzidi maarifa kipa wa Mtibwa na mpira kumpasia Clement Mzize ambaye alifunga bao la tatu dakika ya 81 ya mchezo na kuzua furaha kwa mashabiki wa Yanga sc waliojaa uwanjani hapo ambapo matokeo hayo yalidumu mpaka mwishoni mwa mchezo huo.
Yanga sc sasa jumla imetwaa ubingwa wa ligi kuu nchini kwa mara ya 30 kwa ujumla na ikiwa ni kwa mara ya tatu mfululizo ambapo pia inawania kuingia fainali ya kombe la shirikisho la Crdb.