Klabu ya Yanga sc imezidi kujiimarisha kileleni mwa msimamo wa ligi kuu nchini baada ya kupata ushindi wa 1-0 katika mchezo wa ligi kuu dhidi ya Geita Gold Fc uliofanyika katika uwanja wa Chamazi jijini Dar es salaam.
Yanga sc iliingia katika mchezo huo ikiwa bila mastaa wengi wa kikosi cha kwanza kama Khalid Aucho ambaye ni majeruhi,Pacome Zouzou,Mudathir Yahaya,Ibrahim Hamad ambao mwalimu Gamondi aliamua kuwapumzisha kwa ajili ya maandalizi ya kuikabili Azam Fc siku ya jumapili machi 17.
Augustine Okrah aliwahadaa walinzi wa Geita Gold Sc na kupiga pasi iliyomkuta Azizi Ki ambaye alipiga shuti kali lililomshinda kipa Costa Jn na kuandikia Yanga sc bao la kwanza na bao pekee la mchezo huo dakika ya 28 kipindi cha kwanza.
Licha ya Yanga sc kujitahidi kuongeza mabao lakini hawakufanikiwa huku Joseph Guede,Kennedy Musonda,Aziz Ki na Clement Mzize wakikosa nafasi kadhaa za wazi kutokana na kukosa umakini wa kumalizia mipira waliyopasiwa.
Yanga sc sasa imefikisha alama 52 kileleni mwa msimamo wa ligi kuu ya Nbc baada ya kucheza michezo 19 ya ligi kuu huku Geita Gold Fc wenyewe wakisalia na alama 21 baada ya kucheza michezo 21 ya ligi kuu huku wakiwa katika nafasi ya 14 ya msimamo wa ligi kuu sehemu ambayo inahatarisha nafasi yao ya kubaki ligi kuu msimu ujao.