Klabu ya Yanga sc imekubali kichapo cha mabao 2-0 kutoka kwa Al Hilal Fc ya nchini Sudan katika mchezo wa kwanza wa michuano ya klabu bingwa barani Afrika hatua ya makundi uliofanyika katika uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.
Ukiwa ni mchezo wa kwanza wa Kocha Sead Ramovic baada ya kuajiriwa klabuni hapo,Yanga sc ilianza mchezo kwa kasi ikijitahidi kupata bao la mapema lakini kadri muda ulivyozidi kwenda ilianza kukosa pumzi na stamina ilianza kushuka na kusababisha Al Hilal kurudi mchezoni.
Prince Dube na Stephan Aziz Ki waliokua wanaongoza mashambulizi kikosini humo walikosa ufanisi na kuufanya mchezo kwenda mapumziko ikiwa 0-0.
Kipindi cha pili Al Hilal Fc waliamua kuanza kushambulia wakiwazidi maarifa viungo wa Yanga sc wakiongozwa na Mudathir Yahaya na Duke Abuya walioshika dimba huku Khalid Aucho akikosekana kutokana na kuwa majeruhi.
Juhudi binafsi za winga Adama Coulibary ziliipatia Al Hilal Fc bao la uongozi baada ya kumzidi maarifa Ibrahim Hamad Bacca na kumpiga tobo kipa Djigui Diarra dakika ya 63 ya mchezo huo na kuwafanya Yanga sc kuwa watumwa wa mchezo huo wakitafuta ushindi kwa nguvu zote.
Licha ya mwalimu Sead Ramovic kuwaingiza Cletous Chama na Kennedy Musonda bado mchezo ulikua mgumu kwa Yanga sc ambapo walijisahau na kushambulia kwa nguvu bila kuchukua tahadhari hali iliyofanya kifungwa bao la pili dakika ya 90 ya mchezo kupitia kwa Yassir Mozamil aliyewazidi mbio walinzi wa Yanga sc.
Yanga sc sasa imepoteza michezo mitatu mfululizo msimu huu ikipoteza michezo miwili ya ligi kuu dhidi ya Azam Fc na Tabora United na huu wa ligi ya mabingwa huku Jumamosi itawavaa Namungo Fc ugenini Ruangwa.
Katika msimamo wa kundi A la hatua ya makundi ya michuano ya klabu bingwa barani Afrika Al Hilal Fc ipo kileleni ikiwa na alama tatu huku Mc Algers na Tp Mazembe zikifuatana baada ya kutoa sare huku Yanga sc ikiwa mkiani mwa kundi hilo.