Mshambuliaji raia wa Burkina Faso Yacouba Songne ametamani kurudi nchini kucheza katika ligi kuu ya Nbc kutokana na kuvutiwa na ushindani mkali uliopo katika ligi kuu nchini tofauti na huku alipo sasa nchini Djibout.
Yacouba mchezaji wa zamani wa Yanga sc alijiunga na klabu ya Arta Solar 7 ya nchini Djibout na kuikacha klabu ya Ihefu ambapo kwa mujibu wake ni kuwa alivutiwa na donge nono analolipata nchini humo tofauti na alivyokua bongo.
Hata hivyo Yacouba amesema kuwa licha ya fedha kuwa nyingi bado ligi kuu ya nchi hiyo haina ushindani wa kutosha tofauti na ya hapa nchini ambayo ina ushindani wa kutosha.
Yacouba alisema ameanza hesabu upya za kurejea nchini kucheza, akivizia dirisha dogo litakalofunguliwa katikati ya mwezi huu na kufungwa Januari 15 mwakani, ili aje kuendeleza ule moto kwa lengo la kulinda kipaji chake badala ya kuendelea kucheza ligi nyepesi huku akivuna fedha za kutosha.
“Ligi ya huku sio ngumu kabisa, nakubaliana kwamba malipo yao ni tofauti na Tanzania kwa kile nilichokuwa nalipwa, lakini hapa unaweza kufifisha kipaji, hawa hawachezi soka la ushindani mkubwa,”.
Tayari mchezaji huyo ameanza mawasiliano na baadhi ya klabu za ligi kuu nchini ili arejee kujiunga nazo ambapo kama mazungumzo yakikaa sawa basi tutarajie kumuona nchini mwezi januari.