Rais wa heshima wa klabu ya Simba sc Mohamed Dewji amerejea katika Uongozi wa klabu hiyo kama Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Klabu hiyo akichukua nafasi ya Dk.Salim Abdalah Muhene “Try Again” ambaye amejiuzuru nafasi hiyo huku akimteua kuwa mjumbe wa bodi ya wakurugenzi wa klabu hiyo yenye makazi yake Msimbazi Kariakoo jijini Dar es salaam.
Awali Try Again alitangaza kujiuru nafasi yake ya Mwenyekiti wa Bodi ya wakurugenzi ya klabu hiyo akisema kuwa kujiuru huko ni kwa manufaa makubwa ya klabu hiyo huku akimuomba Dewji akubali kuchukua nafasi yake kama Mwenyeketi wa Bodi ili kuiendesha klabu hiyo kwa weledi zaidi na kuleta mshikamano.
“Nimemuomba Mwekezaji wetu Mo Dewji aje kuwa Mwenyekiti wa Bodi, ninaona yeye ndiye mtu pekee anayeweza kuipeleka Simba mbali, mimi nitaendelea kuwa shabiki na mwanachama halali wa klabu.”Alisema Try Again wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kujiuzuru kwake.
Bosi huyo wa karibu na Tajiri Mohamed Dewji alisema kuwa katika miaka saba akiwa kama mjumbe na Mwenyekiti wa Bodi hiyo klabu hiyo imepata mafanikio mbalimbali ikiwemo kuchukua makombe takribani 17 huku akisisitiza kuwa pia kuna changamoto mbalimbali bado zipo ambazo zinasababisha timu hiyo kushindwa kufanya vizuri katika kipindi cha misimu mitatu iliyopita.
Baada ya Try Again kujiuzuru nafasi hiyo usiku Mohemd Dewji alitangaza kukubali kurejea klabuni hapo kama Mwenyekiti wa bodi ya klabu hiyo akisema amefikia uamuzi huo baada ya kuombwa na Try Again huku akitafakari na kujadiliana kwa kina na Jaji Mihayo ambaye aliongoza mchakato wa mfumo wa mabadiliko ya klabu hiyo.
“Ninarejea nikiwa na nguvu na ari mpya mpaka Simba itakaporejea kwenye hali yake ya kawaida huku naongozwa zaidi na ushabiki wa Simba, siyo uwekezaji, wala ufadhili wala udhamini hivyo sitaiacha Simba leo wala kesho”.Alisema Dewji akizungumza kupitia mtandao wake wa Instagram.
Pia Dewji amesema amemuomba Salim aendelee kuwa mjumbe wa bodi, ombi ambalo limekubaliwa, na hivi karibuni atatangaza wajumbe wengine watakaounda bodi hiyo ili kuisimamisha upya Simba huku akitaja kuwa klabu hiyo ilikua inakabiliwa na changamoto nyingi kama vile kutokua na Umoja,Kukosa timu yenye ushindani,Usajili Mbovu,mfumo duni wa kukusanya wanachama wapya, Kutokuwepo kwa mkakati wa ukuzaji na uendelezaji wa vijana pamoja na Miundombinu iliyoko Bunju kutokidhi mahitaji.
Mohamed ameahidi kutatua changamoto hizo kwa kushirikiana na wenzake huku akiwataka wanasimba wote kuwa kitu kimoja, kumpa ushirikiano, kuzika tofauti zao na kuepuka migogoro.