Kocha wa klabu ya Yanga Sc Miguel Gamondi amesema kwamba bado mashabiki wa Yanga Sc wasitegemee uwepo wa Pacome ZouZoua kwani bado hajawa sawa kwa asilimia 100% na anaweza kuwepo katika mchezo wa kombe la Shirikisho dhidi ya Tabora United ama wategemee mchezaji huo kumuona kwenye mchezo mwingine
Gamondi amesema hayo mapema hii leo alipokua katika mkutano na waandishi wa habari kuelekea mchezo huo wa robo fainali ya kombe la shirikisho la Crdb ambapo katika mahojiano kadhaa Pacome Zouzoua yeye alisema kuwa yupo tayari kuitumikia Yanga kwakuwa anaendelea vizuri.
Pia Meneja wa Yanga,Walter Harrison alinukuliwa akisema Pacome Zouzoua na Joyce Lomalisa wanaendelea vizuri kiafya na ni suala la Mwalimu kuamua kuwatumia na kuzua matumaini makubwa ya mashabiki wa klabu ya Yanga sc huenda wakamuona staa huyo baada ya kumkosa zaidi ya mwezi mmoja na nusu sasa.
Kocha Miguel Gamondi mbali na hilo amesisitiza kuhusu umuhimu wa kuwaheshimu wapinzani pamoja na kupata ushindi katika mchezo huo ili kufuzu hatua ya nusu fainali.
“Ni mchezo wa robo fainali, tunafahamu hatua kama hizi mechi zinakuwa ngumu. Tunajua ubora wa mpinzani wetu hivyo tunapaswa kujiandaa vyema kwa ajili ya dakika 90” Alisema Miguel Gamondi
“Ni kweli nakumbana na changamoto ya timu ambazo zinakaa sana nyuma lakini haimaanishi hatupati matokeo, tumecheza na timu nyingi ambazo zinakaa nyuma na kupoteza muda lakini najua uwezo wa wachezaji wangu, tupo tayari kucheza katika mazingira yoyote. Jambo la muhimu ni kucheza kwa utulivu na kutumia nafasi chache zinazopatikana” Alisitiza Kocha Miguel Gamondi
Mchezo huo unatarajiwa kufanyika kesho saa mbili usiku katika uwanja wa Chamazi Complex jijini Dar es salaam ambapo mshindi katika mchezo huo atakutana na mshindi katika ya Geita Gold Sc dhidi Coastal Union.