Klabu ya Simba sc imelazimishwa sare ya 2-2 na Namungo Fc katika mchezo wa ligi kuu ya soka ya Nbc uliofanyika katika uwanja wa Majaliwa Wilayani Ruangwa mkoani Lindi na kuzua gumzo miongoni wa wadau kuhusu mstakabari wa Simba sc katika mbio za ubingwa msimu huu.
Simba sc ikicheza bila mastaa wake Cletous Chama,Saido Ntibanzokiza,Henock Inonga Bacca na Shomari Kapombe ambao ni majeruhi ambapo kocha Juma Mgunda aliamua kuanza na Edwin Balua,Kibu Dennis na Leandre Onana katika eneo la kiungo cha ushambuliaji ambapo Onana alifunga bao zuri la kuongoza kwa shuti kali lililomshinda kipa Ndikumana dakika ya 34 ya mchezo.
Bao hilo halikudumu sana kwani dakika ya 39 Kelvin Sabato alisawazisha kwa kichwa akiunganisha faulo iliyopigwa vizuri na mpira kumshinda kipa Ayoub Lakred ambapo mpaka mapumziko matokeo yalibaki 1-1.
Kipindi cha pili dakika ya 70 Edwin Balua alipiga faulo kali na kuipatia Simba sc bao la pili ambalo lilifufua matumaini ya kupata alama tatu kwa Simba sc lakini makosa binafsi ya mlinzi Kennedy Juma yalisababisha Namungo Fc wapate bao baada ya mchezaji huyo kujifunga dakika ya mwishoni mwa mchezo.
Mpaka dakika 90 zinakamilika matokeo yalibaki 2-2 ambapo Simba sc sasa imefikisha alama 47 baada ya michezo 22 katika nafasi ya tatu ya msimamo wa ligi kuu huku Namungo Fc ikiwa katika nafasi ya tisa ikiwa na alama 27 katika michezo 24 ya ligi kuu ya Nbc.