Connect with us

Makala

Miqquisone Atemwa Simba Sc

Klabu ya Simba sc imetangaza uamuzi mgumu wa kuachana na mchezaji Luis Miqquisone ambaye alitua klabuni hapo msimu uliopita baada ya mkataba wa mchezaji huyo kumalizika na klabu kuamua kutomuongeza mkataba mpya staa huyo raia wa Msumbiji.

Simba Sc ilimsajili mchezaji huyo kwa mara ya pili baada ya kuvunja mkataba wake na klabu ya Al ahly iliyomsajili kutokea klabuni hapo lakini hakupata nafasi ya kutosha ya kucheza na punde baada ya kurejea Simba sc bado mchezaji huyo alishindwa kuonyesha kiwango cha kutosha na kuishia benchi.

Kocha Roberto Oliveira “Robertinho” hakuvutiwa na kiwango cha Miqquisone ambaye alionekana kuwa na uzito zaidi na hivyo kupungua kasi yake ya mchezo ambapo hata alipokuja kocha Abdelhack Benchika bado hakumtumia ipasavyo winga huyo kwani mara nyingi alimpa dakika chache.

Simba sc wakati inamsajili staa huyo ilimpa mkataba wa mwaka mmoja wenye kipengele cha kufanya tathmini ya kiwango chake ili kuamua kama aongezewe mwingine ama la na baada ya msimu kuisha klabu haikutaka kuendelea na staa huyo.

Tayari mchezaji huyo ameishaondoka nchini kwenda nyumbani kwao Msumbiji akisubiri kujiunga na timu nyingine huku akisisitiza kuwa hana mpango wa kurudi tena kucheza soka nchini Tanzania.

“Ni kweli sitakuwa Simba SC, kama ambavyo klabu imetangaza leo (jana), naomba msiumie. Ndio maisha ya soka yalivyo, mimi nitabaki kuwa shabiki wa Simba SC na mashabiki wa Simba SC nitawakumbuka wakibaki moyoni mwangu.”Alisema staa huyo.

“Hapana sitacheza tena Tanzania, nimeshaondoka huko hivi sasa ninavyoongea nanyi, nipo kwangu Msumbiji hapa Tete. Sitacheza timu yoyote Tanzania, mtajua hivi karibuni wapi nitakwenda, nitawatangazia hapa.”Alimalizia kusema kupitia teknolojia ya video mtandaoni.

Kuachwa kwa mchezaji huyo kumepokelewa tofauti na mashabiki wa soka nchini huku wengine wakiunga mkono uamuzi wa klabu hiyo na wengine wakiona kama alikua anapaswa kupewa muda zaidi wa kucheza na anakua ni mchezaji wa nne kuachwa baada ya John Bocco,Saido Ntibanzokiza na Shabani Idd Chilunda.

Click to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

More in Makala