Imefahamika kuwa mchezaji Lameck Lawi ataitumikia klabu ya Coastal Union baada ya mabosi wa klabu hiyo kufikia makubaliano na klabu ya Simba sc ili mchezaji huyo asalie klabuni hapo.
Awali ilifahamika kuwa mchezaji huyo alisaini Simba sc lakini kutokana na kukiukwa kwa baadhi ya vipengele vya makubaliano basi mabosi wa klabu hiyo waliamua kumpeleka nje ya nchi kwa ajili ya kufanya majaribio ambapo dili hilo lilifeli na mchezaji kurudi nchini.
Kufuatia tukio hilo klabu hizo ziliingia mgogoro ambao ulipelekwa katika kamati ya usajili na hadhi za wachezaji ya shirikisho la soka nchini ambapo kamati hiyo iliamuru klabu hizo zijadiliane zenyewe ili zifikie muafaka na kama ikishindikana basi ingeingilia kati ambapo baada ya vikao kadhaa sasa vilabu hivyo vimamalizana rasmi.
“Suala la Lawi limekuwa na maswali mengi sana, lakini majibu yake yatapatikana Septemba 13, mwaka huu tutakapomtumia katika mchezo wetu dhidi ya Mashujaa FC, hapo tutakuwa tumejibu kila kitu tulichoulizwa, hili jambo limeshamalizika, huyu kwa sasa ni mchezaji halali wa Coastal Union”.Amesema Afisa habari wa klabu ya Coastal Union aliyefahamika kwa jina la El Sabri
“Ni kweli Simba wamekuwa waungwana, tumekaa nao vikao viwili na tumekubaliana, uungwana ndiyo unaotakiwa kwenye mpira, nasi pia tunawashukuru wenzetu, sisi pia tunaahidi tutafanya uungwana zaidi kwao, tunawashukuru sana,”Alimalizia kusema
Kutokana na hilo sasa ni rasmi Lawi anabaki katika klabu yake ya awali na mpaka sasa tayari ameshaanza mazoezi na klabu hiyo kujiandaa na mchezo dhidi ya Mashujaa Fc.