Bodi ya Wadhamini ya klabu ya Yanga sc chini ya Mwenyekiti wake Mhe.George Mkuchika limetakiwa kuachia ngazi na mahakama ya hakimu mkazi Kisutu kutokana na katiba iliyowaingiza madarakati kutotambulika kufuatia wadai kushinda kesi ya msingi iliyofunguliwa mwaka 2022.
Hukumu hiyo inayowaondoa madarakani bodi hiyo ya wadhamini ambayo mbali na Mwenyekiti Mh.Mkuchika pia inaundwa na wajumbe Mama Fatma Karume,Mh.Mwigulu Lameck Nchemba,Mh.Abbas Tarimba na Mh.Anthony Mavunde kufuatia kesi iliyofunguliwa Agosti 4 2022 na walalamika Godfrey Mwaipopo na Juma Ally wakitaka kutombulika kwa baraza hilo kufuatia katiba ya mwaka 2010 iliyowaingiza madarakani kuwa batili.
Mbali na madai hayo pia walalamikaji waliomba wakabidhiwe miamala yote ya fedha sambamba na kuiendesha klabu hiyo wao wenyewe baada ya bodi hiyo kuwa batili kisheria huku ikiitaka bodi iliyokua madarakani kwa katiba ya 1968 kurudi kuendesha klabu hiyo.
Walalamikaji hao baada ya hukumu hiyo kutolewa mwaka jana,mwaka huu walirudi mahakamani kukazia hukumu hiyo kisha taarifa hizo kusambaa na kuzua taharuki nchini hasa kwa mashabiki wa Yanga sc.
Baada ya taarifa hizo kusambaa klabu ya Yanga sc kupitia kwa mkurugenzi wake wa Sheria Wakili Simon Patrick wamefanya mkutano na vyombo vya habari kujibu kuhusu suala hilo ambapo alikiri ni kweli lipo na tayari wamepokea hukumu hiyo na wanaifanyia kazi kutokana na kutofahamu tangu awali kuhusu uwepo wa kesi hiyo.
“Mnamo tarehe 6/11/2022 watu wawili waliojiita Wanachama wa Young Africans SC walifungua kesi Mahakama ya Kisutu, Bwana. Juma Ally pamoja na Geofrey Mwipopo. Walifungua kesi dhidi ya Wajumbe wa Baraza la Wadhamini ambao ni Mama yetu Fatma Karume, Abeid Mohamed Abeid na Mzee Jabir Katundu kwa madai ya kuwa hawalitambui baraza la wadhamini la Klabu ya Young Africans SC, wakidai liliingia kwa mujibu wa Katiba ya 2010(ambayo wanadai haijasajiliwa)”.Alisema Simon mbele ya Waandishi wa habari.
“Kutokana na kutoitambua katiba ya 2010, wanadai wanachama wote si halali, hivyo na Viongozi wote na uanachama wao ambao wanauita wa Katiba ya 2010 ni batili, kwa maana Rais wa Klabu, Makamu wake, Wajumbe wa Kamati ya Utendaji, Viongozi wote walioajiriwa kwa kigezo cha uanachama ni batili pamoja na kazi zote zilizofanywa na Viongozi wote waliopo madarakani nazo ni batili na wanataka ripoti ya fedha na matumizi wakabidhiwe”.Aliendelea kusema Simon Patrick,Mkurugenzi wa Sheria wa Young Africans Sc.
Simon alisema kuwa baada ya kufahamu hayo klabu hiyo imeomba mapitio upya wa kesi hiyo kutokana na kushirikisha upande mmoja huku pia kukiwa na jinai baada ya wadai kufoji sahihi za viongozi wa klabu hiyo.
“Klabu tumegundua kuwa, Abedi Mohamed Abedi aligushi sahihi za Mama Fatma Karume, alighushi sahihi Jabir Katundu ambaye alilazimishwa na sahihi ya Mzee Mkuchika. Mzee Jabir Katundu alituma barua yake Kisutu akieleza kuwa hakuwahi kusaini chochote kinachohusiana na kesi hiyo hivyo Klabu imeomba Mahakama iongeze muda wa Klabu kufanya mapitio ya kesi kwani Klabu haikuwahi kushiriki kwenye kesi hiyo,Klabu vile vile itaomba mahakama ifuatilie jinai ambazo zimeonekana kwenye kesi hiyo ikiwemo kughushi sahihi za baadhi ya Viongozi waandamizi wa Young Africans SC”.Alimalizi kwa kusema Simon Patrick.
Yanga sc kwa miaka ya hivi karibuni imekua mfano wa kuigwa kutokana na klabu hiyo kutokua na migogoro ya mara kwa mara hali ilisababisha kufanya vizuri ndani na nje ya mipaka ya nchi.