Vinara wa ligi kuu bara klabu ya Azam FC wanatarajia kuweka kambi ya wiki mbili visiwani Zanzibar kujiandaa na mechi za Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) ambazo zinatarajiwa kurejea punde tu baada ya michuano ya Afcon kumalizika.
Mabosi wa Azam Fc wanaamini kuwa Visiwani humo ni mahali sahihi kwa timu kujiandaa na ligi kuu ambapo wapo kileleni mwa msimamo licha ya kuwa wana mechi nyingi zaidi kuwashinda Simba sc na Yanga sc ambao wana viporo vya michezo kadhaa.
“kambi hiyo itakuwa maalumu kwa ajili ya kulisaidia benchi letu la ufundi, kujenga muunganiko mzuri kwa wachezaji wetu, ambao kwasasa wametawanyika baada ya mapumziko mafupi waliyopewa tangu tulipotolewa Kombe la Mapinduzi.”Alisema mkuu wa Idara ya habari ya klabu hiyo Zakaria Thabit.
“Tutaingia kambini Januari 23 tukianzia Azam Complex kwa siku mbili kisha tutakwenda Zanzibar kumalizia maandalizi hayo na baada ya hapo tutakuwa tayari kwa mechi za Ligi Kuu na mashindano mengine,” Alimalizia kusema bosi huyo maarufu kama Zaka Za kazi.
Msimu huu Azam Fc imepania kurejesha heshima yake ikianza kwa kufanya usajili wa maana mwanzoni mwa msimu na sasa kipindi hiki cha dirisha dogo tayari wameongezwa mastaa wawili kutoka nchini Colombia ambao ni beki na kiungo mshambuliaji.