Klabu ya Yanga sc imefanikiwa kufuzu hatua ya makundi ya kombe la shirikisho barani Afrika baada ya kuifunga klabu ya Club Africains ya nchini Tunisia kwa 1-0 katika mchezo uliofanyika nchini humo katika uwanja wa Hammedi Agrebi Olympic Stadium uliopo jijini Tunis.
Ikianza na viungo wenye asili ya kushambulia Khalid Aucho,Salum Abubakar na Feisal Salum huku mawinga wakiwa na Jesus Moloko,Benard Morrison na mshambuliaji akiwa ni Fiston Kalala Mayele Yanga sc ilicheza kwa nidhamu ya hali ya juu wakati wa kushambulia na kuzui wakiongozwa na safu ya ulinzi iliyokua chini ya Dickson Job,Yannick Bangala,Kibwana Shomari na Joyce Lomalisa.
Yanga sc ilifanikiwa kumaliza kipindi cha kwanza kwa suluhu kutokana na Club Africains kuwa waoga katika kufunguka na kuwa wanashambulia kwa kushtukiza huku wakikaba kwa pamoja na kuwapa muda mzuri Yanga sc kucheza bila presha yeyote hasa ikichangiwa na utulivu wa Sure Boy eneo la katikati mwa uwanja.
Stephane Aziz Ki aliingia kuchukua nafasi ya Khalid Aucho na kuongeza idadi ya washambuliaji eneo la mbele ambapo mpira aliouanzisha kwenda kwa Farid Mussa ulirejeshwa kwa Sure Boy aliyepiga krosi iliyomkuta Mayele na kumtulizia yeye mwenyewe Ki ambaye alipiga shuti kali la chini lililomshinda kipa wa Africains na kuwapa Yanga sc bao la uongozi dakika ya 79 ambalo lilidumu mpaka dakika ya mwisho ya mchezo.
Yanga sc kutokana na ushindi huo wa ugenini sasa imefuzu kwemda hatua ya makundi ya kombe la shirikisho kwa jumla ya matokeo ya 1-0 baada ya kutoka suluhu katika mchezo wa awali uliofanyika nchini Tanzania.