Mpaka sasa sintofahamu imetawala miongoni mwa wadau wa soka nchini kutokana na kutofanyika kwa mchezo baina ya Yanga sc dhidi ya Simba sc siku ya Jumamosi machi 8 2024 ambapo mpaka sasa hatma ya mchezo huo haijulikana itakuwaje.
Mchezo huo namba 184 uliahirishwa na bodi ya ligi kuu nchini kutokana na klabu ya Simba sc kutoa taarifa kupitia mitandao yake ya kijamii wakisema kuwa hawatashiriki mchezo huo baada ya kuzuiwa kufanya mazoezi siku ya machi 7 saa moja jioni kama ulivyo utaratibu wa kikanuni wa kawaida ambapo timu ngeni hupewa nafasi ya kufanya mazoezi katika uwanja wa mechi siku moja kabla ya mchezo huo.

Hata hivyo Pamoja na simba sc kutoa taarifa hiyo bado bodi ya ligi kuu nchini asubuhi ya machi 8 2024 ilisisitiza kuwa bado mchezo huo upo kama ilivyopangwa ambapo pia klabu ya Yanga sc nayo ilitoa taarifa kuwa mchezo huo upo kama ilivyopangwa na haitocheza mchezo mwingine tofauti na huo wa machi 8 huku ikiwasisitiza mashabiki kukata tiketi kwa wingi.

Mchana wa machi 8 2024 bodi ya ligi ilitoa tena taarifa ya kuahirisha mchezo huo baada ya kukaa kikao na kuamua kutoa uamuzi huo ambapo bado ulileta sintofahamu baada ya mashabiki baadhi kuwa wameshakata tiketi na maandalizi mengi yakiwa yamefanyika ikiwemo wadhamini Azamtv ambao walikua wameshafunga mitambo yao kwa ajili ya kuonyesha mchezo huo moja kwa moja.

Yanga sc walieendelea na maandalizi kuelekea mchezo huo licha ya taarifa hiyo huku kikosi kikiingia uwanjani hapo saa 11 jioni kwa ajili ya kupasha misuli moto ambapo walijkuta wakiwa pekeyao bila waamuzi,wasimamizi wa mchezo huo Pamoja na timu pinzani yaani Simba sc.
Mpaka sasa msimamo wa bodi ya ligi ni kuwa wataupangia mchezo huo tarehe nyingine ambapo pia klabu ya Simba sc wanasubiria tarehe hiyo ya mchezo huo kufanyika na wakati huo huo msimamo wa klabu ya Yanga sc ni kuwa wapewe alama tatu na mabao matatu ambapo pia hawatakubali mchezo huo kupangiwa tarehe nyingine kama wanavyotaka bodi ya ligi kuu nchini.