Klabu ya Simba sc imeshindwa kuibuka na alama tatu katika mchezo wa ligi kuu dhidi ya Azam Fc uliofanyika katika uwanja wa Azam Complex Chamazi jijini Dar es salaam baada ya mchezo kumalizika kwa sare ya 1-1.
Katika mchezo huo uliokua na kasi huku timu zote zikishambuliana kwa zamu,Azam Fc iliingia na mfumo wa mabeki watatu,viungo watano na washambuliaji wawili hali iliyowapa ugumu Simba sc ambao walikua na mabeki wanne,viungo wakabaji wawili na viungo washambuliaji watatu na straika akisimama John Boko.
Mabao ya mchezo huo yalipatikana kipindi cha kwanza ambapo Rodgers Kola alifunga dakika ya 37 kwa upande wa Azam FC kisha lile la Simba lilifungwa na John Bocco mwishoni mwa kipindi cha kwanza na kufanya kwenye msako wa pointi tatu wagawane pointi mojamoja mpaka mwisho wa mchezo.
”Tumekuwa kwenye mwendo ambao hatujaupenda na tulipata nafasi mbele ya Azam FC lakini tumekwama kuzitumia hili ni tatizo,Ubora wa safu ya ushambuliaji kutoweza kutumia nafasi ambazo tumezitengeneza ni sababu ya kushindwa kupata matokeo, kwa hili tutalifanyia kazi kwa mechi zijazo,”Alisema Pablo Franco kocha wa klabu ya Simba sc.
Simba sc sasa imwefikisha alama 5o katika michezo 24 ikiwa katika nafasi ya pili ya msimamo wa ligi kuu nchini huku Azam Fc ikiwa katika nafasi ya tano ikiwa na alama 33 katika michezo 24 ya ligi kuu.