Mabao mawili ya mshambuliaji Lionel Ateba yameiokoa klabu ya Simba Sc na kuondoka na alama tatu katika mchezo wa ligi kuu ya Nbc nchini dhidi ya Mashujaa Fc uliofanyika katika uwanja wa Kmc Complex Jijini Dar es Salaam Mei 2 2025.
Katika mchezo huo wa kiporo ulioahirishwa hapo nyuma kutokana na Simba Sc kuwa na ratiba ya michuano ya kombe la Shirikisho barani Afrika ulishuhudiwa bao la mapema la Mashujaa Fc likipatikana dakika ya 6 ya mchezo kwa shuti kali la Jafary Kibaya lililomshinda kipa Moussa Camara.
Mashujaa Fc baada ya bao hilo walikaa nyuma muda mwingi wa mchezo wakilinda ushindi huo mpaka kipindi cha kwanza kinatamatika.

Kocha Fadlu Davis alifanya mabadiliko na kuwaingiza Mohammed Hussein na Shomari Kapombe pamoja na Kibu Dennis aliwapumzisha Valentino Nouma,David Kameta na Edwin Balua ambapo Simba sc walipata penati baada ya beki wa Mashujaa Fc kuunawa mpira dakika ya 65 iliyofungwa na Lionel Ateba.
Mashujaa Fc walipata pigo baada ya kipa Patrick Muntary kupata kadi ya pili ya njano na kupewa nyekundu dakika ya 78 ya mchezo huo.
Dakika tisini za mwamuzi zilipokaribia kutokana na upotevu mkubwa wa muda alilazimika kuongeza dakika 15 ambapo Simba sc walipata penati ya pili baada ya Shomari Kapombe kuangushwa na Ateba kufunga penati hiyo dakika ya 90+19.
Simba sc sasa imefikisha alama 60 ikicheza michezo 23 ya ligi kuu ya Nbc huku Yanga sc ikiwa kileleni na alama 70 katika michezo 26 na Mashujaa Fc ikiwa na alama 30 katika michezo 27 ya ligi kuu.