Timu ya Taifa ya Senegal imefanikiwa kufuzu michuano ya kombe la dunia nchini Qatar baada ya kuifunga Misri kwa bao 1-0 katika mchezo wa marudiano uliofanyika katika uwanja wa Abdoulaye Wade nchini Senegal.
Goli la kujifunga la Hamdi Faith dakika ya nne lilifanya mzani ukae sawa kwa pande zote mbili ukizingatia katika mchezo wa awali Misri ilishinda bao 1-0 huku katika mchezo huu wa pili Misri walibanwa pande zote za uwanja na kumfanya Mo salah kushindwa kufurukuta dakika zote tisini ambapo Senegal walikosa mabao ya wazi huku faulo zikitawala na kufanya wachezaji wengi wa Misri kuhitaji matibabu na wengine kufanyiwa mabadiliko.
Misri walionekana kuhitaji kwenda katika changamoto ya matuta hasa kutokana na namna walivyocheza kipindi cha pili huku ubora wa golikipa Mohamed El Shenawy ukiwaokoa mara kadhaa kiasi cha kufanikiwa kumaliza dakika 90 pamoja na 30 za nyongeza.
Changamoto ya mikwaju ya penati ilipelekea manahodha wote wawili Mo salah na Khalidou Koulibary kukosa penati za kwanza huku timu zote zikikosa penati za pili kabla ya Ismaila Sarr na El Solia kufunga penati zao kwa pande zote mbili na kisha Bamba Dieng akifunga na Benjamin Mendy akionesha ubora kwa kucheza penati ya Mostafa Mohamed na Sadio Mane alifunga penati ya mwisho kwa shuti kali akimuacha kipa El Shenawy akishangaa.
Senegal imefanikiwa kufuzu kwenda kombe la dunia ikiungana na Ghana,Tunisia,Morroco na Cameroon kutimiza timu tano zitakazowakilisha bara la Afrika katika michuano hiyo mikubwa duniani.