Timu ya Taifa ya Morroco imeishangaza dunia baada ya kufanikiwa kuwaondosha katika michuano ya kombe la dunia nchi ya Hispania kwa kuifunga mabao 3-0 katika changamoto za mikwaju ya penati baada ya kumaliza dakika 90 na 30 za nyongeza bila bao.
Awali mwanzoni mwa mchezo huo Morroco inayonolewa na kocha mzawa Walid Regragui iliiheshimu Hispania inayonolewa na kocha wa zamani wa Barcelona Luis Enrique baada ya kuamua kukaa nyuma wakijilinda zaidi na kuwaachia Hispania Umiliki wa mpira huku wakishambulia kwa kushtukiza.
Nidhamu hiyo ya ulinzi ilifanikisha Morocco kumaliza salama dakika 90 za mchezo huku wakikosa nafasi kama tatu za wazi kupitia kwa mshambuliaji wao mkuu Youssef En-Nesyri anaichezea Sevila Fc ya nchini Hispania.
Baada ya dakika za nyongeza mwamuzi aliamuru changamoto ya mikwaju ya penati ambapo kipa wa Morroco Bono alipangua mikwaju ya Carlos Soler na Sergio Busquets huku mkwaju wa kwanza wa Pablo Sarabia ukigonga nguzo na kwa upande wa Morroco mastaa kama Abdelhamid Sabiri,Hakim Ziyech na Achraf Hakim wakifunga penati zao huku beki wa klabu ya Al ahly ya Misri Badr Benoun akikosa.
Sasa baada ya kufuzu hatua ya robo fainali kwa mara ya kwanza Morocco wataivaa Ureno katika hatua ya robo fainali ambapo mechi za hatua hiyo zitaanza siku ya Ijumaa na Jumamosi ndio siku ya mchezo husika.