Klabu ya Manchester United imefanikiwa kuifunga Arsenal 3-1 katika mchezo wa ligi kuu uliofanyika katika uwanja wa Old Trafford ambapo mabao ya Antony pamoja na Marcus Rashfod yalitosha kuchukua alama tatu na kuipandisha Man Utd katika nafasi ya tano ya msimamo wa ligi kuu nchini humo.
Arsenal ilipata bao la mapema dakika ya 14 lakini mwamuzi alikataa bao hilo ambapo dakika ya 35 usajili mpya wa klabu hiyo Antony alifanikiwa kufunga bao lake la kwanza katika mechi yake ya kwanza ya ligi kuu nchini Uingereza akipokea pasi nzuri kutoka kwa Marcus Rashford dakika ya 35 bao ambalo halikudumu sana kwani Arsenal walisawazisha kupitia kwa Bukayo Saka mapema kipindi cha pili.
Dakika sita baadae Marcus Rashford alifunga bao zuri la pili kwa Man united akipokea pasi ya Bruno Fernandes huku pia dakika nane baadae yaani dakika ya 74 Christian Erriksen alitoa pasi safi kwa Rashford na kuandika bao la tatu ambalo lilikamilisha kalamu ya mabao kwa Man United.
Man utd sasa imepanda juu katika nafasi ya tano ya msimamo wa ligi kuu nchini humo ikiwa na alama 12 katika michezo sita huku Arsenal wakisalia kileleni wakiwa na alama 15 katika michezo sita ya ligi kuu huku wakiwa na michezo migumu mfululizo mbele yao dhidi ya Manchester City,Liverpool na Tottenham.