Kiungo wa klabu ya Yanga sc Feisal Salum ameinyamazisha klabu ya Simba sc baada ya kufanikiwa kufunga bao katika ushindi wa 1-0 ilioupata Yanga sc dhidi ya Simba sc katikam mchezo wa nusu fainali ya michuano ya kombe la shirikisho la Azam uliofanyika katika uwanja wa Ccm Kirumba jijini Mwanza.
Kocha Nasreddine Nabi aliwashtukiza wadau wa michezo alipoamua kutumia washambuliaji wawili katika mfumo wa 3-5-2 akiwaanzisha pamoja Fiston Mayele na Herritier Makambo huku akiaanzisha viungo watatu waliosaidiwa na mabeki wa pembeni waliocheza kama mawinga hali iliyowapa wakati mgumu Thaddeo Lwanga,Sadio Kanoute na Mzamiru Yassin waliocheza eneo la katikati mwa uwanja.
Dakika ya 24 ya mchezo Feisal Salum alipokea pasi kutoka kwa Salum Abubakar na kufumua shuti lililojaa wavuni moja kwa moja na kuandika bao la kwanza na la ushindi kwa Yanga sc.
Licha ya Simba sc kujitahidi kusawazisha bao hilo lakini walibanwa vilivyo eneo la umaliziaji ambako iliwaanzisha Kibu Dennis,Pappe Sakho na Chris Mugalu huku wakikosa nafasi ya kusawazisha baada ya kichwa cha Joash Onyango kugonga mwamba wa juu.
Yanga sc sasa inasubiri mshindi kati ya Azam fc na Coastal Union ili kujua itakutana na nani katika mchezo wa fainali utakaofanyika katika uwanja wa Sheik Amri Abeid jijini Arusha.