Licha ya kuwa na malalamiko kuhusu kushuka kiwango tangu asajiliwe na klabu ya Yanga sc Stephane Azizi Ki amefanikiwa kuwafunga midomo wote waliokuwa na shaka juu ya uwezo wake baada ya kufunga mabao matatu katika ushindi wa 5-0 wa Yanga sc dhidi ya Kagera Sugar Fc.
Yanga sc ilikua na wakati mzuri katika mchezo huo wakishambulia mara kwa mara huku Fiston Mayele akikosa mabao ya wazi mapema kipindi cha kwanza lakini juhudi zake zilizaa matunda baada ya mabeki wa Kagera wakiongozwa na Abdalah Mfuko kumchezea madhambi na mwamuzi kuamuru iwe penati iliyofungwa kiufundi na Aziz Ki dakika ya 43.
Dakika mbili baadae Aziz Ki tena alipiga shuti kali akiwa umbali wa takribani mita 40 kutoka golini na kumchumgulia kipa wa Kagera Sugar Said Kipao aliyeruka bila mafanikio.
Fiston Mayele alifunga bao lake la 16 katika ligi kuu msimu huu akimalizia kazi yake nzuri baada ya kuwakimbiza mabeki wa Kagera dakika ya 50 ambapo baadae alimpisha Walid Mzize huku Zawadi Mauya na Tuisila Kisinda wakiwapisha Mudathir Yahya na Kennedy Musonda.
Bernard Morrison aliyechukua nafasi ya Farid Musa alifunga bao la nne dakika ya 85 akimalizia pasi safi ya Aziz Ki huku pia kiungo huyo akifunga bao la tatu kwake na la tano kwa Yanga sc kwa penati baada ya Mzize kuangushwa katika eneo la hatari.
Yanga sc sasa imeendelea kujichimbia kileleni mwa msimamo ikiwa na alama 68 huku Simba sc ikiwa nafasi ya pili ikiwa na alama 60 ambapo timu hizo zitavaana siku ya Jumapili April 16 mchezo ambao unaweza kuwahisha ama kuchelewwesha ubingwa kwa Yanga sc.