Ni aibu baada ya klabu ya Azam Fc kukubali kipigo cha mabao 3-1 kutoka kwa Namungo Fc katika uwanja wa nyumbani siku ya Ijumaa katika mchezo wa ligi kuu ya Nbc.
Mchezo huo ambao matokeo hayo hayakutarajiwa kutokana na mwenendo wa Azam Fc msimu huu ambapo katika mchezo sita walikua wameshinda michezo minne huku wakifungwa mmoja na kutoa sare moja huku Namungo Fc wakiwa hawajaonja ushindi wowote katika ligi kuu msimu huu.
Azam Fc walikua na mabadiliko machache katika kikosi kilichoipa upinzani mkubwa Yanga sc siku ya Jumatatu ambapo mshambuliaji Allasane Diarra alianza badala ya Prince Dube huku Namungo nao wakimpumzisha kipa Deogratius Munishi.
Pius Buswita alikua na siku nzuri kazini akifunga bao kwa kichwa dakika ya 10 ya mchezo huku Hashim Manyanya aliongeza bao la pili dakika ya 19 na kipindi cha pili dakika ya 50 Reliants Lusajo aliandikia Namungo Fc bao la tatu kwa baada ya timu hiyo kufanya shambulizi la ghafla langoni mwa Azam Fc.
Bao la kufutia machozi la Azam Fc lilifungwa na Ayoub Lyanga dakika ya 70 ya mchezo ambapo pamoja na jitihada za Azam Fc kutaka kusawazisha mabao mawili lakini uimara wa safu ya ulinzi ya Namungo Fc ikiongozwa na kipa Jonathan Nahimana ulikua vizuri.
Sasa Azam Fc wamesalia katika nafasi ya tatu na alama 13 huku Namungo Fc wakipanda mpaka nafasi ya 12 wakiwa na alama 6 katika michezo saba ya ligi kuu nchini.