Kiungo wa klabu ya Yanga sc Khalid Aucho anatarajiwa kuwa nje ya uwanja kwa takribani wiki tatu akijitibu majeraha ya nyama za paja aliyoyapata katika mchezo wa ligi kuu ya Nbc nchini dhidi ya Coastal Union.
Kiungo huyo aliumia na kulazimika kutomaliza mchezo huo baada ya kupata majaraha hayo na nafasi yake kuchukuliwa na Mudathir Yahaya katika mchezo ambao Yanga sc iliibuka na ushindi wa 1-0.
Taarifa rasmi kutoka kwa madaktari wa klabu ya Yanga sc wakiongozwa na Daktari mkuu wa klabu hiyo imebainisha kuwa baada ya Kiungo huyo kufanyiwa vipimo ilibainika atakua nje kwa muda huo.
“Ni kweli Aucho amefanyiwa vipimo katika Hospitali ya Saifee jijini Dar es Salaam na kubainika kuwa na majeraha ya nyama za paja na hivyo tutamkosa kwa takribani wiki tatu”,Alisema Ally Kamwe msemaje wa klabu ya Yanga sc akithibitisha uwepo wa taarifa hiyo kutoka idara ya matibabu ya klabu hiyo.

Kukosekana kwa Aucho kunamaanisha kuwa sasa Mudathir Yahaya pamoja na Duke Abuya watakua na kazi ya kupambana kuhakikisha klabu hiyo inapata alama tatu katika mchezo wa ligi kuu ya Nbc dhidi Azam Fc utakaofanyika kesho April 10 2025 katika uwanja wa Azam Complex Chamazi jijini Dar es Salaam.
Yanga sc yenye alama 61 kileleni mwa msimamo inataka kuendelea kukaa kileleni huku Azam Fc iliyokatika nafasi ya tatu ya msimamo nayo inataka kujihakikishia nafasi ya kushiriki michuano ya kimataifa mwakani.