Timu ya Taifa ya Argentina imefanikiwa kutwaa taji la tatu la kombe la Dunia baada ya kuifunga Ufaransa kwa mikwaju ya Penati 4-2 baada ya kumaliza dakika 120 wakifungana 3-3 huku Lionel Messi akifunga mara mbili na Kylian Mbappe akifunga mabao matatu(Hatrick) katika mchezo huo wa kusisimua.
Iliwachukua Agentina dakika 23 kuandika bao la kwanza baada ya Angel Di Maria kuangushwa ndani ya eneo la hatari na mwamuzi kuamuru penati ambayo ilifungwa na Lionel Messi kisha Messi alihusika tena katika kutengeneza bao la pili lililofungwa na Di Maria dakika ya 36 ambapo mpaka hapo matumaini ya Argentina kutwaa taji hilo yalianza kuonekana.
Dakika ya 81 Kylian Mbappe alifunga kwa penati kisha dakika moja baadae akafunga tena na kufanya mchezo kumalizika kwa 2-2 ambapo mchezo ulihamia katika dakika 30 za nyongeza ambapo Messi alifunga bao la tatu kwa timu yake dakika ya 108 lakini Mbappe alisawazisha tena kwa penati dakika ya 118 na kuufanya mchezo uuingie katika changamoto ya matuta.
Kipa Emiliano Martinez aliokoa penati ya Kingsley Coman huku Aurelien Tchouameni akishindwa kulenga lango na kuwapa nafasi argentina kutwaa taji hilo la tatu na kukata kiu ya Lionel Messi ya kutwaa taji la kombe la Dunia.
“Nilihitaji sana taji hilo katika maisha yangu maana ndio lilikua pekee ninalikosa na sasa siwezi kuomba kitu kingine”Alisema Messi ambaye ameichezea timu yake ya taifa michezo 172.