Klabu ya Simba imekiri kuwa mambo ni magumu na hakuna uwezekano wa kuwazidi kete watani wao Yanga sc katika mbio za kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya NBC msimu huu ambao wameachwa kwa alama 13 mpaka sasa.
Kauli hiyo imetolewa leo na meneja Habari wa Simba, Ahmed Ally katika mkutano na waandishi wa habari jijini Mwanza huku akitamba kuwa kwa kutambua hilo wameelekeza nguvu zote kwenye mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam ili kufuta machungu ya mambo magumu waliyoyapitia msimu huu.
Simba itavaana na Yanga Jumamosi katika mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Shirikisho utakaopigwa Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza saa 9:30 alasiri.
Ahmed Ally amesema kuchukua kombe hilo klabu itakuwa imetikimiza asilimia 70 ya malengo yake msimu huu baada ya mambo kuwaendea kombo kwenye Ligi Kuu ya Nbc ambako uhakika wa kutwaa taji ni mdogo.
“Maandalizi yanakwenda vizuri ni mchezo wetu wa maana na wa thamani kubwa unakwenda kufuta machungu tuliyopitia msimu huu,Ligi kuu mambo yanazidi kuwa magumu mpinzani wetu anazidi kulisogelea kombe lakini huku (Shirikisho) bado ni kweupe kuchukua taji hili tutakuwa tumetimiza asilimia 70 ya malengo yetu ya msimamo,”Amesema msemaji wa Simba Sc,Ahmed Ally.
“Licha ya Yanga kujipambanua kuwa timu bora msimu huu lakini Wekundu wa Msimbazi kinaamini katika ubora wa kikosi chake kwani mechi za namna hiyo ndizo Simba anapenda kuzicheza huku akiwaomba mashabiki kujitokeza kwa wingi ili kuisaidia timu kutimiza malengo yake”