Kiungo wa Simba, Jonas Mkude, ni miongoni mwa wachezaji 26 waliyoondoka Dar es Salaam jana asubuhi Juni 22 kuelekea Mbeya kwa ajili ya mechi mbili muhimu za ugenini.
Mkude bado hajaichezea Simba tangu Ligi Kuu Bara irudi baada ya kusimama kwa miezi mitatu kutokana na janga la virusi vya corona.
Kiungo wetu alipata majeraha na kukimbizwa hospitali kwa matibabu zaidi baada ya kuumia katika mechi ya kirafiki dhidi ya KMC uliyochezwa Uwanja wa Mo Simb Arena.
Taarifa za awali za matibabu zilionyesha Mkude atakua nje ya uwanja kwa wiki mbili huku akiendelea kufanya mazoezi binafsi.
Daktari wa Simba, Yassin Gembe, alithibitisha Mkude ni miongoni mwa wachezaji waliochaguliwa na kocha, Sven Vandenbroeck, kwa safari ya Mbeya.
“Kocha ndiye atakayeamua kama atamtumia Mkude baada ya kujiridhisha na utimamu wake wa mwili kutokana na mazoezi aliyofanya tangu alipopata jeraha katika mchezo wa kirafiki,” alisema Dkt. Gembe.
Wachezaji ambao wameachwa Dar es Salaam kwa programu maalumu ni beki Tairone dos Santos na straika Cyprian Kipenye huku Sharaf Shiboub akiwa bado nchini kwao Sudan kutokana na marufuku ya kutotoka nje yaliyosababishwa na corona.
Simba wanawakabili Mbeya City Jumatano Juni 24 na baadaye Juni 28 dhidi ya Tanzania Prisons mechi zote zikipigwa Uwanja wa Sokoine.
Cc:Simbausajili