Mshambuliaji wa klabu ya Mashujaa Fc Ismail Mgunda amerejea nchini baada ya dili lake kujiunga na klabu ya As Vita ya nchini Dr Congo kufeli kwa sababu za kimaslahi.
Mgunda alimvutia kocha Yousouph Dabo wa As Vita ambaye aliuagiza uongozi wa klabu hiyo kumsajili staa ambapo dili lilielekea kuzuri kiasi cha Mshambuliaji huyo kusafiri kwenda nchini Congo kwa kumalizia mazungumzo ya mwisho na kusaini mkataba.
Hata hivyo dili hilo limeshindwa kufanikiwa kutokana na As Vita kutoweka ofa ya maana ili kununua mkataba wa mwaka mmoja na nusu wa staa huyo uliosalia klabuni hapo.
Uongozi wa Mashujaa Fc umesema kuwa muda wowote endapo As Vita wataweka kiasi kinachohitajika basi staa huyo atajiunga na timu hiyo.
“Ishu ni maslahi kwa sababu mchezaji huyo bado ana mkataba wa mwaka mmoja na nusu, hata mkimuuliza atasema, hivyo lazima timu ipate maslahi kwa kuuzwa kwake, ikishindikana basi tutakuwa hatuna namna nyingine atarejea tutaendelea kumpa ushirikiano wa kazi kama kawaida, maana wakati anaondoka hakutoroka aliaga kabisa,” kilisema chanzo hicho.
Hata hivyo alipotafutwa Mgunda alikiri kuwa dili hilo lipo matatani kutokana na masuala ya maslahi na hana budi kurejea klabuni hapo.
“Narejea katika timu ya Mashujaa maana ni mchezaji wao nina mkataba wa mwaka mmoja na nusu, hivyo siwezi kuzungumza zaidi ya hilo.”Alisema Mgunda
Mgunda amekua na mchezaji aliyeonyesha kiwango bora zaidi katika safu ya ushambuliaji ya klabu hiyo huku kasi yake na nguvu ikiwa ni silaha kubwa dhidi ya mabeki wa timu pinzani.