Kocha mkuu wa klabu ya Yanga sc Miguel Gamondi amezuia uwezekano wa staa wa klabu hiyo Maxi Nzengeli kuondoka klabuni hapo kujiunga na timu ya Kaizer Chiefs ambayo imeonyesha nia ya wazi kumsajili nyota huyo baada ya kuvutiwa na kiwango chake katika mchezo dhidi ya Fc Augusburg ya nchini Ujerumani.
Mabosi wa Kaizer baada ya kumuona Nzengeli alipokiwasha katika mchezo huo moja kwa moja walianza kuulizia uwezekano wa kumsajili katika dirisha hili huku wakipanga kutumia ukaribu wao na mabosi wa Yanga sc kukamilisha dili hilo mapema.
Gamondi baada ya kusikia taarifa hiyo aligeuka mbogo akisema kuwa hana mpango wala hataruhusu staa wake yeyote yule aondoke klabuni hapo kwa msimu huu kwa maana hesabu za usajili tayari alishazifunga na sasa ana kazi ya kutafuta muunganiko wa kimbinu.
“Sitakubali kumkosa mchezaji ambaye yuko katika kikosi kwa sasa, ruhusa pekee nitakayotoa ni pale atakapokosekana kwa sababu za majeraha na sio kumuuza,” alisema Gamondi na kuongeza kuwa
“Kikosi tulichosajili ni kwa malengo yetu ya msimu ujao kwa ajili ya mashindano ya kimataifa na ya ndani, hivyo haiwezekani kumpunguza hata mmoja, ijapokuwa nafahamu zinakuja ofa nyingi kwa wachezaji wetu nyota, lakini hatukuruhusu waondoke na badala yake tulipambana kuwabakiza ili kulinda hesabu za msimu ujao.”Alimalizia kusema
Nzengeli amegeuka lulu nchini tangu ajiunge na Yanga sc akitokea katika klabu ya As Maniema ya nchini Congo Drc ambapo alikua akifanya vizuri kiasi cha kuchukua tuzo ya mchezaji bora msimu wa 2023/2023.