Bao la Cletous Chama dakika ya 33 ya kipindi cha kwanza limeifanya Simba sc kuibuka na ushindi wa alama tatu katika mchezo wa ligi kuu baina ya timu hiyo dhidi ya Jkt Tanzania uliofanyika katika uwanja wa Meja Isamuhyo ulioko mbweni jijini Dar es salaam.
Ikianza na Fredy Michael kama mshambuliaji Simba sc ilizidiwa hasa eneo la kiungo na kuruhusu mashambulizi mara kadhaa lakini uimara wa kipa Ayoub Lakred ulisababisha Jkt washindwe kupata bao.
Chama aliyeshiriki katika mashambulizi mengi ya Simba sc alifunga bao la pekee katika mchezo huo kwa shuti kali baada ya kupokea pasi nzuri ya Saido Ntibanzokiza na kufunga kwa shuti hilo lililomshinda kipa wa Jkt tanzania dakika ya 33 ya mchezo.
Chama tangu arejee kutoka Afcon alipokua na timu ya Taifa ya Zambia amecheza jumla ya mechi nne ambapo katika mechi hizo, Mwamba huyo wa Lusaka ameshacheka na nyavu mara mbili akifunga kwenye mchezo dhidi ya Azam FC na dhidi ya JKT Tanzania.
Mbali na magoli, Chama ametoa pasi mbili zilizozaa magoli. Pasi hizo alitoa kwenye mchezo dhidi ya Tabora United ambapo Simba ilishinda magoli 4-0.
Simba sc sasa imekamilisha mzunguko wa kwanza wa ligi kuu ya Nbc nchini ikiwa imecheza michezo 15 ikiwa na alama 36 katika nafasi ya pili ya msimamo huku Yanga sc akiwa kileleni na alama 40.