Ni furaha na huzuni zimetawala jijini Dar es salaam kufuatia klabu ya Yanga sc kuifunga Simba sc mabao 5-1 katika mchezo wa ligi kuu nchini uliofanyika katika uwanja wa Benjamini Mkapa jijini Dar es salaam jumapili ya Novemba 5,2023.
Awali pamoja na kuwepo kwa mvua kubwa tangu alfajiri ilitarajiwa kuwa mchezo huo utakua mgumu kwa pande zote huku Simba sc akipewa nafasi ya kushinda mchezo huo kutokana na uzoefu wake wa kucheza katika hali ya mvua kubwa huku Yanga sc wakipewa nafasi ndogo ya kuibuka na ushindi.
Waalimu Roberto Oliveira na Miguel Gamondi kila mmoja alianza na kikosi chake cha kila siku ambacho kila mmoja aliamini kinampa matokeo chanya katika mchezo huo huku mshangao mkubwa kwa mashabiki ni kuanza kwa kipa Aishi Manula aliyekua na majeraha ya muda mrefu huku safu ya ulinzi ikiwa na Shomari Kapombe,Mohamed Hussein,Henock Inonga na Che Fondoh Malone huku eneo la kiungo likiwa na Sadio Kanoute,Fabrice Ngoma,Saido Ntibanzonkiza,Cletous Chama na Kibu Dennis huku mshambuliaji akiwa ni Jean Baleke.
Yanga sc wakiwa na mfumo wa 4-2-3-1 walianza na Djigui Diarra huku mabeki wakiwa ni Yao Yao,Joyce Lomalisa,Dickson Job na Ibrahim Hamad huku kiungo wa chini wakiwa ni Khalid Aucho na Mudathir Yahya huku eneo la huu wakicheza Maxi Nzengeli,Pacome Zouzou pamoja na Stephane Aziz Ki na mshambuliaji akiwa ni Kennedy Musonda pekee.
Iliwachukua Yanga sc dakika tatu kuandika bao la kwanza likifungwa na Kennedy Musonda aliyeunganisha krosi ya Yao Yao bao ambalo lilikuja kusawazishwa na Kibu Dennis kwa kichwa dakika ya tisa akimalizia kona ya Saido Ntibanzokiza matokeo ambayo yalisalia mpaka kipindi cha kwanza kinamalizika.

Kipindi cha pili Yanga sc iliamka na kufanikiwa kupata mabao mawili ya haraka haraka hasa baada ya kuingia Clement Mzize ambaye aliwavuruga mabeki wa Simba sc kutokana na kuwa na kasi ambapo pasi ya Aziz Ki ilimaliziwa vizuri na Nzegeli na kuipa Yanga sc bao la pili dakika ya 64 huku tena Mzize akimpasi pasi nzuri Aziz Ki na kufunga bao zuri dakika ya 73 ya mchezo.

Nzengeli alifunga tena bao la nne kwa Yanga sc dakika ya 77 akimalizia kazi nzuri ya Mzize ambaye aliwahadaa mabeki baada ya kupokea pasi ya Pacome Zouzou huku kasi ya Nzengeli tena ikiwafanya Yanga sc wapate penati baada ya kuuwahi mpira wa Aziz Ki ambao ulikua unaambaa na kumfanya Henock Inonga kucheza faulo na mwamuzi Ahmed Arajiga kuweka penati iliyofungwa na Pacome Zouzou.

Kutokana na ushindi huo sasa Yanga sc imefikisha alama 21 katika nafasi ya kwanza ya ligi kuu baada ya michezo nane huku Azam Fc ikiwa katika nafasi ya pili ya msimamo ikiwa na alama 19 ikiwa imecheza michezo tisa huku Simba sc ikiwa katika nafasi ya tatu ikiwa na alama 18 katika michezo saba ya ligi kuu nchini.