Klabu ya Simba sc ina wakati mgumu kuelekea mchezo wa marudiano wa michuano ya African Footbal League nchini Misri dhidi ya Al Ahly baada ya kutoka sare ya 2-2 katika mchezo wa awali uliofanyika nchini katika uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.
Simba inayohitaji ushindi wa aina yoyote au sare ya mabao kuanzia 3-3 ili isonge mbele, haijawahi kuitoa Al Ahly wala kupata ushindi dhidi yao wakiwa Misri katika shindano lolote walilowahi kukutana na hii itakuwa mara ya kwanza iwapo wakifanya hivyo.
Katika ardhi ya Msiri, Simba imekutana na Al Ahly mara tatu ambapo imepoteza zote pasipo kufunga bao hata moja huku ikiruhusu nyavu zake kutikiswa mara nane.
Mfungaji wa bao la kwanza la Simba sc kwenye mechi ya mkondo wa kwanza iliyopigwa kwa Mkapa Ijumaa iliyopita, Kibu Denis amesema “Ahly ni timu kubwa lakini hata sisi ni wakubwa, kila kitu kinawezekana kwenye soka. Tuna timu nzuri na kila mchezaji anajituma huku tukiwa na ushirikiano wa kutosha.”
“Zitakuwa ni dakika 90 za nguvu, tutapambana hadi mwisho na lengo ni kutinga nusu fainali.”Alisema Kibu Dennis
Endapo Simba sc ikiingia nusu fainali itakuwa na uhakika wa kupata Dola 1.7 milioni (Sh4.2 bilioni) ambazo timu inayofika hapo ina uhakika wa kupata kutoka waandaaji wa mashindano hayo.