Kocha mkuu wa klabu ya US Monastir Darko Novic ameukubali ubora wa washambuliaji wawili wa Yanga sc Fiston Mayele na Kennedy Musonda ambao walisababisha apoteze 2-0 katika mchezo wa raundi ya tano ya kombe la shirikisho barani Afrika.
Kocha huyo aliyasema hayo hivi karibuni wakati kikosi chake kikiondoka nchini baada ya kumalizika kwa mchezo ambao umewafanya Monastr kushuka mpaka nafasi ya pili katika msimamo wa kundi D.
Kocha huyo mbali na kuwakubali wachezaji hao pia aliukubali mziki wa kocha Nasredine Nabi hasa kimbinu na kukiri kwamba alipata shida kumsoma tangu mchezo wa kwanza kule nchini Tunisia.
“Tulipocheza na Yanga tukashinda (2-0) lakini muda wote hatukuwa na utulivu wa kuona kama tumemaliza mechi. Nawaheshimu sana (Yanga) kwa kuwa wanaonesha kuna kazi kubwa kocha wao amefanya.. Hata nilipokuwa nawafuatilia na kuangalia mechi zao sikuona kama kuna mchezo wamezidiwa umiliki wa mpira”.
“Silaha ya pili ya Yanga ni wale washambuliaji wawili kwenye eneo la mbele, yule namba 9 (Mayele) ni hatari anajua sana kufunga lakini pia anakasi. Kuna yule jezi namba 25 (Musonda) ndio tatizo zaidi, unapokuwa na washambuliaji wa namna ile wanawalazimisha mabeki kupoteza nidhamu yao kutokana na kasi yao. Kitu kibaya zaidi wanacheza kwa ushirikiano mkubwa”Alisema kocha huyo.
Mayele na Musonda wameanza kuelewena katika eneo la ushambuliaji la timu hiyo hasa baada ya kocha Nabi kuamua kubadili mbinu siku za karibuni akiwatumia wote wawili eneo la mbele huku mmoja akitokea pembeni kiasi cha kuchangia upatikanaji wa mabao nane katika kombe la shirikisho hatua ya makundi.