Shirikisho la soka barani Afrika (Caf) limevitaka vilabu vinavyoshiriki michuano ya kimataifa msimu ujao kukamilisha usajili wa wachezaji mpaka kufikia juni 30 mwaka huu viwe vimetuma orodha katika shirikisho hilo huku likisema halitatoa muda zaidi wa nyongeza.
kauli hiyo ya Caf ni kama imevibana vilabu vya Simba sc na Yanga sc ambavyo vina uhakika wa kushiriki michuano ya kimataifa hapa nchini kwani mpaka wakati huo ratiba ya soka nchini itakua bado inaendelea ambapo Yanga sc watavaana na Coastal Union katika mchezo wa fainali ya kombe la shirikisho jijini Arusha huku dirisha la usajili litakua bado halijafunguliwa kwa hapa nchini.
Kwa mujibu wa ratiba hiyo ya Caf kuna vilabu hapa nchini vinaweza kushindwa kukamilisha usajili huo kama Coastal union ambao endapo watacheza na Yanga sc na kushinda taji hilo watakua wamejikatia tiketi ya kushiriki michuano ya kimataifa lakini watakua tayari wamechelewa kufanya usajili kwa maana inawapasa kusubiri mpaka Julai 2 kupata uhakika kama wana nafasi ya kimataifa huku usajili wa Caf utakua umefungwa tangu Juni 30 mwaka huu.
Pia vilabu vya Simba sc na Yanga sc navyo vina wakati mgumu kwani vinahitaji muda wa kufanya usajili wa baadhi ya wachezaji huku mpaka sasa dirisha la usajili nchini likiwa bado halijafunguliwa.
Hali hii pia iliiathiri klabu ya Yanga sc msimu uliopita ambapo walitolewa na River United ya Nigeria huku wakiwakosa wachezaji nyota klabuni hapo kama Fiston Mayele,Djuma Shabani na Khalid Aucho.